Klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya shilingi laki tano kutokana na vurugu za washabiki wake ikiwemo kurusha mawe na chupa uwanjani katika mechi ya namba 199 iliyowakutanisha na Yanga SC iliyofanyika Aprili 22, 2018 kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya.

Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa na Mtendaji mkuu wa Bodi Ligi Boniface Wambura na kusema Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Saa 72) ya Bodi ya Ligi katika kikao chake kilichokaa mnamo Mei 1, 2018 chini ya Mwenyekiti wake Clement Sanga kiliweza kupitia taarifa na matukio mbalimbali na kukuta baadhi ya vitu vikiwa vimetendeka ndivyo sivyo na kuamua kutoa maamuzi mbalimbali.

"Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na vurugu za washabiki wake ikiwemo kurusha mawe na chupa uwanjani katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 22, 2018 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu", amesema Wambura.

Mbali na hilo, Wambura amesema Kamati imeshindwa kumpa adhabu mchezaji Obrey Chirwa wa Yanga kutokana na waamuzi wa mchezo huo walishampa kadi ya njano kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa Mbeya City ingawa kwenye picha za televisheni inamuonesha kama alimpiga kiwiko.

Kwa upande mwingine, Wambura amesema klabu ya Yanga imeandikiwa barua kuhusu kumuonya mchezaji huyo kwa vile kumbukumbu zinaonyesha ameshafanya matukio ya utovu wa nidhamu mara kadhaa akiwa uwanjani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: