Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret Sitta ameishauri Serikali kuunda chombo huru cha kusimamia elimu nchini ili kuondoa utaratibu uliopo sasa ambapo Serikali ndio msimamizi wa shule zake na shule binafsi.

Akizungumza jana Aprili 30, 2018 wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2018/19, Margaret ambaye alikuwa waziri wa wizara hiyo kwa kipindi cha miaka miwili na nusu katika Serikali ya Awamu ya Nne, amesema chombo hicho kitasaidia kuweka usawa katika elimu.

“Lazima kuwe na chombo maalum cha kusimamia elimu kwa kuchambua sera, lugha za kufundishia kama ni sahihi ama si sahihi, kusimamia mitihani inayotungwa je iendelee kama ilivyo na kutazama mazingira ya shule,” alisema Margaret.

Bajeti ya wizara hiyo ya Sh1.4trilioni imewasilishwa jana asubuhi, wabunge wengi walioijadili waligusia kuanzishwa kwa chombo hicho, baadhi wakibainisha kuwa Serikali imekuwa ikizikandamiza shule binafsi badala ya kuziboresha wakati ikijulikana wazi kuwa shule hizo kwa sasa zinafanya vizuri zaidi kuliko za Serikali.

Margaret pia ameitaka Serikali kuanzisha vyuo zaidi vya maendeleo na ufundi ili vijana zaidi waweze kupata elimu na kujiajiri.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: