Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza kuanza mchakato wa kuyapandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Burigi, Kimisi, Biharamulo, Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa.

Mchakato huo tayari umeungwa mkono na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Hayo yameelezwa juzi bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati akihitimisha mjadala wa bajeti wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

“Mheshimiwa Spika, ninaomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa  Mhe. Rais ameridhia ombi letu la kupandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Burigi, Kimisi, Biharamulo, Ibanda na Chief Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa, kipekee namshukuru sana Mhe. Rais kwa kuridhia ombi letu hilo” amesema Dkt. Kigwangalla.

Amesema kufuatia hatua hiyo, wizara yake inaanzisha mchakato rasmi wa kukamilisha taratibu  za kupandisha hadhi mapori hayo ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii katika kanda ya Kaskazini Magharibi na hivyo kufikia azma ya Serikali kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 8 na mapato ya dola za kimarekani bilioni 16 katika kipindi cha miaka 7 ijayo.

Inaelezwa kuwa mchakato huo utapitia hatua mbalimbali ikiwemo kuwashirikisha wadau husika kupata maoni yao, mapendekezo kuwasilishwa baraza la mawaziri kabla ya kujadiliwa bungeni na hatimaye kuwasilishwa kwa Mhe. Rais kwa ajili ya kuidhinishwa kuwa Sheria kamili ya kupandisha hadhi mapori hayo.

Akizungumzia mikakati mingine mipya ya kuboresha sekta ya maliasili na utalii itakayotekelezwa, Dkt. Kigwangalla amesema ni pamoja na kuanzisha mamlaka ya usimamizi na uendelezaji wa utalii wa fukwe nchini, kuhuisha maeneo ya vivutio vya Mambo ya Kale na kuviunganisha katika ‘package’ moja ya utalii na vivutio vya wanyamapori.

Mikakati mingine ni kuunda mfumo mmoja funganishi wa TEHAMA uitwao “MNRT Portal” kwa ajili ya kutoa leseni na vibali, ukusanyaji wa takwimu na mapato kutoka vyanzo mbalimbali vya sekta ya maliasili na utalii, ambapo utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali iliwemo GePG, NIDA, TIRA, BRELA, TRA na NBS.

Amesema mikakati mingine ni kuanzisha Jeshi Usu, Utambulisho wa Utalii wa Tanzania Kimataifa ujulikanao kama “Tanzania, Unforgettable”, kufungua utalii wa kanda ya kusini, kuanzisha mwezi wa maadhimisho ya Urithi wa Mtanzania “Urithi Festival”  (Septemba), kuhuisha sheria za TANAPA, TAWA na TFS, pamoja na kuunda kanuni mpya za kusimamia vizuri sekta hizo.

Pori la Akiba Burigi lina ukubwa wa kilomita za mraba 2,941 katika wilaya za Karagwe, Muleba na Ngara mkoani Kagera, wakati Pori la Kimisi likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1,030 katika wilaya za Ngara na Karagwe mkoani humo.

Pori la Akiba Biharamulo lina ukubwa wa kilomita za mraba 731 katika wilaya ya Muleba mkoani Kagera na wilaya ya Chato mkoani Geita, huku Pori la Akiba Ibanda likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 200 na Pori la Akiba Rumanyika kilomita za mraba 800 katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.

Mapori haya yapo katika ukanda muhimu wa kuunganisha watalii kutoka ikolojia za Magharibi na Mashariki ambapo uwanja wa ndege wa Chato utakuwa muhimu katika kutoa mawasiliano.

Mapori hayo ambayo yanasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA sasa yatakuwa chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania – TANAPA punde baada ya mchakato wa kuyapandisha hadhi kukamilika.

Bunge limeidhinisha Sh. bilioni 115.794 kwa ajili ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Sh. bilioni 85.816 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh. bilioni 29,978 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: