Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara amepewa onyo kali na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kutoka na yeye kuingia uwanjani kushangilia ushindi wa timu yake mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Simba na Yanga uliochezwa Aprili 29, 2018.
Manara amepewa barua iliyomuonya kutokana na kukiuka sheria za michezo za ligi kuu mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo.
Mtendaji Mkuu wa Bodi Ligi, Boniface Wambura ameeleza kuwa uamuzi huo umeafikiwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichopitia taarifa na matukio mbalimbali ya ligi msimu wa 2017/18 yanayoendelea kulindima hivi sasa, ambapo kilibaini tukio la utovu wa kinidhamu kwa afisa huyo.
“Katika mechi namba 178 dhidi ya Yanga SC iliyochezwa Aprili 29, 2018 katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, mara baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa aliingia uwanjani Haji Manara kushangilia ushindi wa timu yake. Kitendo hicho ni cha ukiukwaji wa Kanuni ya 14(11) ya ligi kuu kuhusu taratibu za mchezo, inayozuia wasiohusika kuingia uwanjani kabla, baada na wakati mechi ikiendelea”, amesema Wambura.
Kwa upande wake, Haji Manara ameonesha kulitambua kosa lake na kuiomba radhi Bodi ya Ligi, Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), pamoja na wadau wote wa soka, huku akieleza kuwa furaha ndiyo iliyompelekea yeye kutenda kosa hilo.
“Muungwana akivuliwa nguo huchutama..naomba radhi bodi ya ligi,TFF na wadau wote..nilihemewa na furaha ndugu zangu..hakuna raha kwangu mm na kwa mshabiki kama kumgalagaza mtani…it will never happen again..ila sijui itakuwaje siku ya kukabidhiwa mwaliπππ @tanfootball #bodiyaligi ππ” ameandika Haji Manara karika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.
Katika Mechi hiyo ambayo ilihudhuriwa namashabiki wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini, Simba iliibuka kidedea baada ya kuichapa Yanga goli 1 ambalo lilifungwa dakika ya 37 na Erasto Nyoni.
Post A Comment: