Mahakama ya Wilaya ya Arumeru imetishia kuifuta kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Shule ya Lucky Vicent na wenzake kwa sababu ya upande wa mashtaka kuomba kesi hiyo iahirishwe mara kwa mara.
Hayo yamesemwa na Hakimu wa mahakama hiyo, Desderi Kamugisha baada ya wakili wa serikali, Alice Mtenga kuomba kesi hiyo iahirishwe hadi tarehe nyingine ili waifanyie mabadiliko hati ya mashtaka.
Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Wakili wa utetezi, Method Kimomogolo alikubaliana na hoja za wakili wa serikali, kwamba kesi hiyo iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Hakimu Kamugisha alikubaliana na ombi la ahirisho la kesi hiyo, huku akiuonya upande wa mashtaka kwamba kama haujajipanga vizuri kuhusu kesi hiyo anaweza kuifuta kwa sababu inaahirishwa mara kwa mara.
Baada ya kusema hayo aliahirisha kesi hiyo hadi leo May 8, 2018 kwa ajili ya kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Post A Comment: