Maandalizi kwa ajili ya uzinduzi wa michezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (Sirro CUP Kibiti 2018) hatua ya 16 bora yamekamilika kwa asilimia tisini na yanatarajiwa kuzinduliwa siku ya Jumatatu na IGP Simon Sirro katika uwanja wa Samora wilayani Kibiti.
Akizungumza wilayani Kibiti baada ya kukagua maandalizi hayo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Barnabas Mwakalukwa amesema lengo la Michezo hiyo ni kuwaweka pamoja wakazi wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji baada ya matatizo yaliyowakumba kumalizika.
“Michezo hii ni fursa nyingine ya kuwakutanisha wakazi wa Wilaya hizi na kuihakikishia dunia kuwa sasa maeneo haya ni salama na Tanzania ni salama baada ya wahalifu waliosumbua hapo awali kudhibitiwa” Alisema Mwakaluka.
Aidha amewaomba wakazi wa maeneo hayo kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia burudani mbalimbali pamoja na maneno ya viongozi mbalimbali yatakayotolewa katika ufunguzi wa michezo hiyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Kombe hilo, Koplo Ramadhan Tamimu amesema michezo hiyo itakapofikia tamati bingwa atajinyakulia kombe na fedha taslimu Milioni moja huku yakichagizwa na kauli mbiu ya “Kibiti Salama, Jamii Salama”
Naye Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kibiti Rashid Mkinga amesema wamejiandaa vyema na anauhakika wa kombe hilo kubaki wilayani Kibiti kwa kuwa pamoja na kuwa na timu bora lakini pia wanatarajia kupata mashabiki wengi.
Ufunguzi huo utapambwa na burudani mbalimbali zikiongozwa na  Bendi ya dansi  ya Jeshi la Polisi, Msanii wa nyimbo za asili Ndolela, Man Prince na vikundi mbalimbali kutoka Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: