Mahakama ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, imemhukumu kifungo cha miaka 3 jela Immani Andongwisye (20), mkazi wa Kijiji cha Katumba Kata ya Kibisi wilayani Rungwe mkoani Mbeya kwa kosa ya kujaribu kumbaka bibi wa miaka 70.

Bibi aliyenusurika kufanyiwa kitendo hicho ametajwa kwa jina la Rahab Salesi, 70 mkazi wa kijiji na kata hiyo.

Akisoma shtaka hilo Jumatano, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo, Patrick Maliyabibi, alidai kwamba mstakiwa huyo alitenda kosa hilo Aprili 18 mwaka huu saa 2:00 usiku alipoingia ndani ya nyumba ya mama huyo.

Alidai mshtakiwa alipoingia ndani alimvua nguo bibi huyo kwa nguvu kisha kuanza kumtomasa tomasa maeneo mbalimbali ya mwili wake, akitaka kumwingilia kimwili, lakini bibi huyo alijiangusha chini kutoka kwenye kitanda.

Maliyabibi aliiambia mahakama kuwa baada ya kujiangusha chini, alichukua panga chini ya uvungu wa kitanda kisha kumkata kidole kijana huyo, ambaye alikimbia.

Baada ya Andongwisye kukimbia, bibi huyo alikwenda kwenye uongozi wa kijiji usiku huo kutoa taarifa ambapo alikamatwa na kupelekwa polisi mjini Tukuyu.

Aliongeza kuwa baada ya kuwekwa lumande alifunguliwa kesi namba 38 na kuanza kusikilizwa katika mahakama hiyo huku mashahidi wa upande wa mashtaka wakipeleka ushahidi.

Mwendesha Mashtaka huyo aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa huyo, ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaofanya vitendo hivyo kwa kuwa suala hilo linawadhalilisha wanawake ambao wengi wao ni wajane.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Aristrida Tarimo, alisema ameridhika na ushahidi iliotolewa na upande wa mashtaka, hivyo kumhukumu kutumikia kifungo cha miaka 3 jela, ili iwe fundisho kwa wengine.

Nje ya mahakama, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Katumba, walisema mahakama imetenda haki kwa kuwa kitendo kilichofanywa na kijana huyo ni cha udhalilishaji.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: