Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wameitaka Serikali kutilia mkazo ushauri uliotolewa na marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wa kuwapo kwa mjadala wa kitaifa wa elimu.
Wakizungumza leo Mei 5, 2018 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, wabunge wa upinzani wamesema hali ya elimu ni mbaya na Serikali inaandaa kizazi kijacho kisichoweza kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia amesema, “Taifa lolote lile ambalo halijui umuhimu au halipendi kuwekeza katika elimu ni Taifa mfu, ukitaka kuua elimu yetu basi usiwekeze katika elimu.”
Mbatia ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa amesema, Taifa hili limebahatika kuwa na marais walimu isipokuwa Mzee Mkapa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni Mwalimu, ‘First Lady’ Janeth Magufuli ni mwalimu.
“Leo Tanzania tupo wapi? Na rasilimali kubwa kuliko zote duniani ni rasilimali watu na rasilimali watu tuliyonayo sasa haijitambui na ili ilijitambue lazima iwe na ufahamu.
“Kama Rais Mkapa anaomba mjadala wa elimu na amekuwa akilirudia mara kwa mara. Rais Kikwete amezungumza haya. Rais Mwinyi amesema nchi inaongozwa kama gari bovu. Mwalimu Nyerere alilisema hadi anaingia kaburini,” amesema Mbatia na kuongeza:
“Tuwe na mjadala mpana wa kitaifa, Tanzania ni yetu sote, watoto hawa wanaumia, hivi ukweli watoto wa rais wetu wanasoma katika shule hizi hizi, hebu tumwogope Mwenyezi Mungu.”
Mbatia amesema vitabu vinavyosambazwa sasa shule za msingi ni vibovu na kumtaka Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako kuacha kutoa vitisho kwa watu kuwa watachukuliwa hatua na badala yake, “ajiulize tatizo lipo wapi, nani kalisababisha.”
Naye Waziri kivuli wa elimu, sayansi na teknolojia, Susan Lyimo amesema; “Hakuna nchi yoyote iliyoendelea pasina kuwekeza katika elimu, lakini kinachofanyika sasa, ingawa Serikali haitaki kusikia ila hali ya elimu ni mbaya.”
Post A Comment: