Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limesema siku za kumkamata mtuhumiwa wa ujambazi anayeteka watu na kuwapora kwa kutumia bunduki bandia na kisu, zinahesabika.
Limesema kuwa mtuhumiwa huyo amenusurika kukamatwa mara mbili baada ya kuwekewa mtego na polisi.
Akizungumza leo Alhamisi Mei 24, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno amesema mtuhumiwa huyo ambaye jina lake halisi halijulikani, anafanya uhalifu kwa kuteka watu na kuwapora mali zao katika barabara ya Kisili-Buhigwe kwenye pori la Kwitanga.
Pori hilo lipo katikati ya kijiji cha Mahembe na Gereza la Kwitanga katika wilaya ya Kigoma.
"Tunaendelea kumsaka na polisi wamemkurupusha mara mbili ikabidi adondoshe bunduki yake chini, kumbe ni ya bandia na ndio anayotumia kupora watu," amesema Ottieno.
“Bunduki hizo bandia zimechongwa kwa kutumia mbao kiasi kwamba mtu akiitazama kwa mbali bila kuichunguza hawezi kutambua kama ni bandia.”
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kupora watu wanaopita barabarani wakiwa kwenye magari, pikipiki, baiskeli na watembea kwa miguu ambapo hunyang'anya simu za mkononi na fedha.
Ottieno ameomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano wa dhati kwa askari ili iwe rahisi kumkamata jambazi huyo.
Post A Comment: