Mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, Frank Joseph amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Mlandizi mkoani Pwani akishtakiwa kwa wizi wa mahindi.
Joseph ambaye tukio la kukamatwa kwake liliibua hisia na mijadala mitandaoni ikidaiwa alishindwa kutua mzigo aliodaiwa kuuiba, alisomewa shtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Nabwike Mbaba.
Mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 124/2018 akidaiwa kuiba mahindi debe moja yenye thamani ya Sh20,000. Baada ya kusomewa shtaka, mshtakiwa huyo alikiri kutenda kosa.
Hakimu Nabwike aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 10 ili kupata maelezo ya mlalamikaji ambaye hakuwepo mahakamani.
Licha ya mahakama kumweleza mshtakiwa kuwa dhamana iko wazi na kumpa sharti la kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh500,000, alishindwa kutimiza sharti hilo hivyo alipelekwa rumande.
Tangu Mei 3, Joseph alikuwa akishikiliwa na polisi mkoani Pwani akituhumiwa kuiba mahindi kwa mkazi wa Mlandizi.
Tukio la wizi huo lilivuta hisia kwa jamii baada ya mshtakiwa huyo kudaiwa kushindwa kutua mzigo uliokuwa begani hadi alipokimbilia polisi na mwenye mali kupigiwa simu, ambapo alifika na ‘kumsaidia’ kuutua.
Post A Comment: