Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro amewaonya watu waliopata msamaha wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa Aprili 26, 2018 wajichunge tabia na matendo yao.

IGP Sirro ametoa onyo hilo jana Mei 24, 2018 mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo vya polisi vya kisasa vya Mburahati, Kiluvya-Gogoni na Mbweni ambavyo vimezinduliwa leo.

"Nia ya Mheshimiwa Rais Magufuli kuwapa msamaha ilikuwa njema lakini kuna baadhi ya watu wameitumia vibaya fursa hiyo na hadi sasa watu watano wamekwishauawa na wananchi. 

"Natoa onyo kwa wote waliopata msamaha na wana nia ya kurejea kwenye matendo yao maovu, ukitoka gerezani kwa msamaha, maana yake umerekebisha mwenendo wako na wananchi wanatarajia uwe hivyo, lakini kama ukifanya vinginevyo, serikali isilaumiwe", amesema IGP Sirro.

Akielezea kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, Kamanda Sirro amesema tangu ashike madaraka hayo, jeshi hilo limewapeleka askari 1,267 kwenye mafunzo ya medani za kivita na kwamba jeshi hilo liko imara.

"Pia tumepeleka askari wa upelelezi zaidi ya 1,000 kwenye mafunzo ya ujuzi na ustadi (skills and knowledge) wa kupeleleza kesi mbalimbali. 

"Baada ya kuwapa mafunzo haya, tunataka kesi za kawaida upelelezi wake uwe umekamilika ndani ya miezi sita na zile kesi kubwa kubwa upelelezi wake uwe umekamilika ndani ya miezi 12. Tunataka kuhakikisha haki za watanzania zinapatikana kwa wakati," amesisitiza Sirro.

Kwa upande mwingine, Kamanda Sirro alitumia fursa hiyo kumshukuru pia Rais Magufuli kwa kuwapatia sh. bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari, kutoa kibali cha ajira kwa askari wapya 1,500 na kuwaruhusu wawapandishe vyeo askari wenye kustahili kuanzia cheo cha Koplo hadi Naibu Kamishna wa Polisi (DCP).
Share To:

msumbanews

Post A Comment: