Na George Binagi
Baraza la robo mwaka la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, limeendelea na vikao vyake kwa kujadili masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Baraza hilo limeketi hii leo ikiwa ni siku yake ya pili na kujadili ajenda sita ikiwemo maswali ya papo kwa hapo pamoja na taarifa ya mapato ya kwa kipindi cha robo mwaka.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Misungwi, Antony Baheme amewahimiza watendaji wa halmashauri hiyo kusimamia vyema suala la ukusanyaji wa mapato ikiwemo kuwaelimisha wanaosimamia zoezi hilo ili kutambua matumizi sahihi ya mashine za kukusanyia mapato na kuiwezesha halmashauri kukusanya mapato stahiki.
Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya Misungwi, Eliurd Mwaiteleke amewataka watendaji kufuatilia orodha ya baadhi ya wakulima ambao wamepata hasara kwenye zao la pamba kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo wadudu ili kuangalia namna ya kuwasamehe madeni yao kutokana na pembejeo za kilimo walizokopeshwa.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkuu wa wilaya ya Misungwi Juma Sweda amewataka madiwani na watendaji wa halmashauri ya Misungwi kuendelea kuwahimiza wananchi kujikita kwenye suala la kilimo cha pamba, dengu pamoja na mazao mengine kulingana na msimu wa kilimo ili kuondokana na uhaba wa mazao ya chakula na biashara huku akiwaonya wanaojihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja kwani hatawavumilia.
Madiwani wa halmashauri hiyo wametaka kuwepo kwa ufuatiliaji wa karibu kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, maji, umeme pamoja na malipo kwa baadhi ya Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji waliosaidia kwenye zoezi la upigaji chapa mifugo kwani baadhi yao bado hawajalipwa stahiki zao.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: