Familia ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), imesema haki anazostahili ndugu yao zikiwamo gharama za matibabu, uchunguzi wa waliomshambulia kwa risasi, zitacheleweshwa kwa muda lakini hatimaye ipo siku atazipata.

Msemaji wa familia hiyo, Wakili Alute Mughwai, alisema hayo jana wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake, jijini hapa.Alisema familia haitachoka kudai haki za Lissu na kinachojitokeza ni kucheleweshwa lakini siku moja itapatikana.

Akizungumzia haki ya kupata matibabu, alinukuu kifungu cha 24 cha Sheria ya Utawala wa Bunge, 2008, kinachotoa haki hiyo kwake na mwenza wake pamoja na watoto wanne na kwamba utaratibu mwingine wowote unaokwenda kinyume unakiuka sheria hiyo.

“Mbunge si mtumishi wa serikali, mbunge ana taratibu zake za kupata matibabu… Bunge kama mhimili unaojitegemea hauna taratibu zingine zaidi nje ya sheria hiyo,” alisema.

Aprili 19, mwaka huu, Spika wa Bunge Job Ndugai, aliliambia bunge linaloendelea mjini Dodoma kuwa, familia ya Lissu haijawasilisha Ofisi ya Bunge nyaraka muhimu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Wizara ya Afya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais.

Alisema iwapo nyaraka hizo zitapatikana, ofisi yake haitasita kuidhinisha malipo ya matibabu yake.Hata hivyo, Wakili Mughwai alisema utaratibu huo haupo katika sheria ya Bunge.

“Unaposema fuata utaratibu wakati mbunge amepigwa risasi na yupo katika hatari ya kufa unataka kupata nini zaidi? Bunge ambalo ni mhimili unaojitegema limekuwa na utaratibu wa kushughulikia mbunge aliye katika hatari ya kufa baada ya kupigwa rasasi?,” alihoji.

“Huo utaratibu haupo…ni lazima ubuniwe utaratibu wa kuendana na hayo mazingira.”

Alisema tangu kushambuliwa kwa Lissu Septemba 7, mwaka jana mjini Dodoma, familia imekuwa na mawasiliano ya muda mrefu na Ofisi ya Bunge kuhusu matibabu ya Lissu, lakini hata mara moja hawajasema wazi kuhusu utaratibu.

“Kama Bunge wangesema tangu mwanzo katika majadiliano yao kuwa hawawezi kugharimia matibabu yake, tungewaambia ‘thank you’ na kusingekuwapo na vikao vya mjadala,” alisema.

Alisema kwa mfano, Februari 1, mwaka huu, walipokea barua ya Bunge iliyowaarifu kuwa wanawasiliana na Wizara ya Afya kuhusu matibabu ya Lissu na baadaye watawaarifu.

“Ni miezi mitatu sasa, Mei 2 familia imeandika barua Ofisi ya Bunge kuomba mrejesho huo na kujua wamefikia wapi,” alisema. Akizungumzia upelelezi wa tukio hilo, Wakili Mughwai alisema miezi minane sasa imepita na wao bado wanapata kiza kikuu.

“Alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana miezi minane iliyopita na walitakiwa kufanya upelelezi wa kuwatia hatiani watuhumiwa,” alisema huku akisisitiza kuwa wataendelea kudai haki ya ndugu yao bungeni na haki kama mwathirika wa kosa la kijinai.

“Tutaendelea kudai haki hizi hadi zitakapopatikana. Tunajua haki ya mtu inacheleweshwa lakini haitapotea,” alisema.

Akizungumzia hali yake alisema anatarajiwa kufanyiwa operesheni ya 20 ya kurekebisha mifupa katika paja la kulia.

Alisema operesheni iliyopita ilifanyika vizuri na sasa yupo kwa uangalizi wa madaktari kwa siku chache zijazo na baada ya hapo ataendelea na mazoezi ya viungo.

Alisema pamoja na operesheni hiyo atafanyiwa operesheni nyingine ndogo kufuatia kuambukizwa vijidudu na pia kunyoosha mfupa katika paja.

Kuhusu kurudi nchini, alisema hata yeye hajui na kama familia pia haijui.

“Wengi wanatuuliza lini atakuja, jibu letu ni hatujui, na sisi ni watu wa kwanza kutaka arudi nyumbani…hilo ni suala la madaktari wanaomtibu.

“Lissu si mtoto mdogo, anahitaji kutibiwa hayo majeraha na akishapona anatamani kurudi nyumbani,” alisema.

Aikana Kauli ya Spika
Wakili Mughwai alikanusha taarifa ya Spika wa Bunge Ndugai aliyedai kuwa gharama za matibabu ya Lissu yanalipwa na Serikali ya Ujerumani.

“Hiyo habari si ya kweli,” alisema huku akiweka bayana kwamba matibabu ya Lissu, weka na posho za kujikimu vinagharimiwa na wasamaria wema.

“Hii habari imetufedhehesha sana kwa namna moja inatuonyesha sisi familia kuwa ni matapeli.

“Athari ya hii taarifa ni kuwaambia watu waliokuwa wanamchangia gharama za matibabu yake waache,” alisema.

Alisema familia wangekuwa watu wa kwanza kabisa kushukuru kwa kumpata mfadhili huyo mkubwa na wangewaomba wananchi waache kumchangia. Alisema Lissu bado yupo hospitalini na anahitaji msaada.

Wakili Mugwai alitoa namba ya akaunti ya Lissu ya CRDB ambayo ni 01J2043045300 yenye jina la Tundu Antiphas Lissu.

Post A Comment: