Baada ya maziko ya Suguta Chacha (27) aliyeuawa kwa madai ya kuchomwa kisu akiwa mikononi mwa polisi katika kituo cha Sirari, wilayani Tarime familia yake imesema itaweka wakili kusimamia kesi ya ndugu yao mahakamani.
Suguta ambaye ni ndugu wa mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche anadaiwa kuuawa kwa kuchomwa kisu na polisi usiku wa kuamkia Aprili 27.
Heche amesema kwamba ndugu yao alifanyiwa kitendo cha kinyama na kubainisha kuwa wataweka wakili ili mtuhumiwa wa mauaji hayo apate hukumu anayostahili.
“Tunajua yupo wakili wa jamhuri atakayesimamia kesi, lakini nasi tutaweka wetu, tunachotaka ni kwa aliyehusika kupata hukumu anayostahili, familia imeshajipanga kwa ajili ya jambo hilo,” alisema Heche.
Alisema kiuhalisia hakuna fidia yoyote wanayoweza kulipwa ikazidi uhai wa ndugu yao, isipokuwa ni kwa mhusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Tunamshukuru Mungu tumemzika salama, hakuna jambo lolote la kushtua lililojitokeza wakati wa shughuli nzima ya kumuhifadhi ndugu yetu. “Watu walijaa, huzuni na simanzi viliutawala msiba huu ambao unatuumiza sana,” alisema Heche
Post A Comment: