Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amesema Kitengo cha Habari cha Bunge hakilazimishwi kutoa taarifa za video za wabunge zinazorekodiwa wakati wakichangia mijadala mbalimbali ndani ya Bunge hilo.
Dk. Tulia ametoa kauli hiyo leo Mei 9, wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema), aliyehoji nani anayetoa amri kwa kitengo hicho kukata kwa asilimia 90 maelezo ya video za wabunge wanaochangia mijadala mbalimbali bungeni.
Lijualikali amesema licha ya kwamba wabunge wanaongozwa kwa kanuni kuzungumza na hakuna amri ya kufuta kauli unayozungumza bungeni hadi mwisho inashangaza kuona kwenye vipande vya video wananyimwa au inakatawa.
“Unapewa ‘hansard’ iliyokamilika, lakini cha ajabu watu hao wa hansard tunapoenda kuomba video zetu ambazo tumeongea humu bungeni, zinakuwa zimekatwa kwa asilimia 90 hawa wanaokata hotuba zetu wanakata kwa amri ya nani, wakati mbunge nimeongea na kiti kimeniruhusu niongee hadi nimemaliza, anayekata, anakata kwa amri ipi na kwa maelekezo ya nani, naomba mwongozo,” amesema.
Akijibu mwongozo huo, Dk. Tulia alisema taarifa rasmi za Bunge huchapwa na mbunge kukabidhiwa, lakini utaratibu wa bunge kutoa clip za wabunge hiyo hutegemea utashi wa kitengo cha habari.
“Kwa hiyo kuna wakati wanaweza wasikupe na hawalazimiki kufanya hivyo, kwa hiyo kama kuna jambo lolote ambalo umeenda kuomba na hawajakamilisha waambie unaomba muda wako wa dakika 10 kama labda wamekupa dakika mbili badala ya 10 waambie unahitaji zote.
“Sasa inategemea ninyi mmetumia utaratibu upi kuzipata hizo taarifa lakini taarifa rasmi za Bunge ni zile zilizoandikwa na si hizi tunazozungumza. Huo ndiyo utaratibu tulio nao,” amesema.
Post A Comment: