Serikali imetenga shilingi bilioni 53.8 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ikiwa ni fedha kwa ajili ya Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu katika Halmashauri zote nchini ambazo zitagawiwa kwa njia ya mikopo kupitia vikundi mbalimbali.
Hayo yameelezwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri TAMISEMI, Joseph Kakunda alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Handeni, Omar Abdallah Kigoda aliyehoji juu ya kiasi gani Serikali inasimamia suala la asilimia 5 ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya Vijana na Kinamama.
“Serikali imeendelea kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinatenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya shilingi bilioni 56.8 zilitengwa na Halmashauri zote nchini, jumla ya shilingi bilioni 17.5 sawa na asilimia 31 zilitolewa kwa vikundi vya Wanawake na Vijana” amesema Mhe. Kakunda.
Kakunda ameendelea kusema kuwa, katika mwaka 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 15.6 sawa na asilimia 27 zilikuwa zimetolewa ambapo jumla ya vikundi 8,672 vya wanawake na vijana vilipatiwa mikopo.
Aidha amesema kuwa, ili kuongeza uwajibikaji katika kutenga na kupeleka fedha za mfuko wa Wanawake na Vijana kwa vikundi husika, Serikali itaweka utaratibu katika sheria ya fedha (Finance Bill) ya mwaka 2018/2019 utakaohakikisha kwamba Halmashauri zote zinatekeleza kikamilifu agizo hilo.
Post A Comment: