MAHAKAMA ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, leo Alhamisi, Mei 24, 2018 imetupilia mbali kesi ya tuhuma za uchochezi iliyokuwa ikimkabili Mdude Nyagali baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kukamilisha upelelezi.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama hiyo, Mhe. Chami amesema anakubaliana na hoja ya wakili wa upande wa utetezi, Wakili Boniface Mwabukusi kuwa upande wa Jamhuri walipewa muda wa mwisho kukamilisha upelelezi lakini haujafanya hivyo Mahakama imeamua kumuachia huru Mdude Nyagali.

Ndugu Nyagali (Sumu ya Nyigu) alikamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe na kupelekwa Dar es salaam ambako alishikiliwa kwa siku 21 akituhumiwa kufanya uchochezi kupitia kwenye ukurasa wa Twitter.

Katika mashtaka hayo polisi walimtuhumu kwamba mnamo Oktoba 13, mwaka jana, kupitia ukurasa wake wa twitter aliandika “Wale waliomshambulia Mhe. Tundu Lissu sio kazi yetu kuwasamehe, ni kazi ya Mungu, lakini kuwakutanisha watu hao na Mungu ni kazi yetu wenyewe,” mwisho wa kunukuu.

Baada ya kuachiwa huru na mahakama hiyo Ndugu Nyagali amemshukuru Mungu, wakili wake, Bw. Mwabukusi, wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Dar es salaam ambao kila siku walifika kituo cha polisi kumpelekea chakula wakiongozwa na Katibu wa Kanda ya Pwani Ndugu Casmir Mabina.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: