Mfanyabiashara wa mitumba Hadija Hassan amefungua kesi ya madai ya matunzo ya mtoto dhidi ya msanii nguli wa muziki wa kizazi kipya, Ali Kiba maarufu kama King Kiba.
Katika kesi hiyo, Hadija anadai jumla ya Sh. milioni 1.41, ikiwamo Sh. 950,000 za ada na Sh. 460,000 za matumizi ya mtoto wa miaka mitano (jina limehifadhiwa kwa sababu za kisheria na kimaadili).
Hadija ambaye ni mfanyabiashara wa mitumba amefungua kesi ya madai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam akidai matunzo kwa mlalamikiwa ambaye ni mzazi mwenzie -King Kiba.
Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani hapo, mlalamikaji anadai kuwa Januari, 2013 katika Hospitali ya Mikocheni, jijini Dar es Salaam alizaa mtoto wa kike ambaye baba yake ni mlalamikiwa.
Alidai kupitia hati hiyo kwamba mlalamikiwa anatakiwa kumhudumia mtoto huyo kwa mahitaji yote muhimu ikiwamo chakula, nguo, elimu na matibabu.
"Kutokana na Sheria ya Watoto ya mwaka 2009, mdaiwa anatakiwa kutoa huduma kila mwezi, chakula Sh. 150,000, matunda Sh. 50,000, chakula cha ziada Sh. 50,000, michezo na burudani za watoto Sh. 100,000, nguo Sh. 60,000 na matibabu Sh. 50,000 ambapo jumla ni Sh. 460,000," alidai mlalamikaji kupitia hati hiyo.
Aidha mlalamikiwa anatakiwa kulipa ada ya shule kwa muhula Sh. 950,000, na anadaiwa aliacha kutoa matunzo hayo kwa mtoto tangu Januari, mwaka huu hivyo anaiomba mahakama imwamuru mdaiwa kutoa matunzo hayo ya Sh. 460,000 kila mwezi na ada.
Pamoja na mambo mengine, mlalamikaji anaomba malipo ya kwanza yatolewe mapema baada ya hukumu, na pia anaiomba mahakama imwamuru King Kiba kumsomesha mtoto, kumnunulia nguo na matibabu ikiwamo kumtafutia bima ya afya.
Pia mlalamikaji anaomba mahakama imwamuru Kiba kulipa gharama za matunzo Sh. 460,000 kuanzia Februari 2017 mpaka siku itakapotolewa hukumu na gharama za kesi ziwe kwa mdaiwa.
Mbali na maombi hayo, Hadija anaomba mahakama itoe amri nyingine yoyote itakayoona inafaa kwa manufaa yake. Kesi imefunguliwa kwa msaada wa Kituo cha Wanawake cha Msaada wa Kisheria (WLAC).
Ali Kiba, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Ali Saleh Kiba amefunguliwa madai hayo ikiwa ni siku chache tangu afunge ndoa iliyopendeza mjini Mombasa Kenya.
Post A Comment: