WAKATI Arsenal ikishuka uwanjani usiku wa jana kukipiga na Altetico Madrid katika nusu fainali ya Europa League, upande wa pili imebainika kuwa kuna utata juu ya taarifa za kujiuzulu kwa Arsene Wenger ndani ya Arsenal.
Awali ilielezwa Wenger ambaye ni kocha wa Arsenal ameamua kuondoka kwa hiyari yake baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka 22 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kumaliza mkataba wake, lakini taarifa za ndani zinaeleza kuwa bosi huyo Mfaransa ametimuliwa na siyo kuwa amemua kuondoka mwenyewe.
Wenger ataondoka Arsenal mwishoni mwa msimu huu lakini katika maelezo yake ya juzi Jumatano alipoulizwa sababu hasa za kuondoka alisema muda hauruhusu na aliondolewa katika nafasi yake hiyo.
“Suala la muda halikuwa upande wangu, halikuwa na maamuzi yangu,” alisema.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa Mfaransa huyo alilazimishwa ajiondoe na klabu itamlipa pauni milioni 9 ikiwa ni malipo ya mshahara wake wa mwaka mmoja uliosalia.
Baada ya Wenger kutoa kauli hiyo na wengi kueleza kuwa ametimuliwa, dakika 30 baadaye klabu ilitoa tamko kuwa Wenger hakueleweka vizuri.
Post A Comment: