Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameombwa aeleze sababu za kuufungia wimbo wa ‘Mwanaume Mashine’ ulioimbwa na Msaga Sumu.
Pendekezo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu leo Aprili 27, 2018 bungeni ambapo amesema kuwa wimbo huo wa ‘Mwanaume mashine’ unamtaja mcheza soka wa klabu ya Simba, Ramadhani Kichuya kitu ambacho kwa mashabiki wa klabu hiyo wangependa kuutumia siku ya Jumapili Aprili 29 kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga.
“Wimbo huo unamtaja mchezaji soka wa timu ya Simba, Ramadhan Kichuya, wapenzi wa timu hiyo wangependa kuusikiliza siku ya Jumapili wakati Simba ikipambana na Yanga katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,” amesema Zungu.
Serikali kupitia Baraza la Sanaa Taifa mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu ilitangaza kuzifungia nyimbo 15 za wasanii wa muziki wa Bongo Fleva ambapo sababu kubwa ilikuwa ni nyimbo hizo kukiuka maadili ya kitanzania.
Hata hivyo, kwenye orodha hiyo wimbo wa ‘Mwanaume Mashine’ haukutajwa na hakuna taarifa rasmi kutoka BASATA za kufungiwa kwa wimbo huo.
Post A Comment: