Leo April 18, 2018 Meneja wa Ofisi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya wameunganishwa katika kesi ya jinai inayomkabili aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzanke wawili.
Mahakama hiyo inatarajia kuanza kusikiliza kesi hiyo mfululizo kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka kuanzia May 14,17 na 21, 2018.
Washtakiwa hao wameunganishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri mara baada ya Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leonard Swai kuomba kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka.
Washtakiwa wamesomewa mashtaka yao upya 30 badala ya 28 yaliyokuwa yakiwakabili awali.
Mbali na Rais TFF, Jamal Emil Malinzi(57) wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine(46) na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawayo Mwanga(27).
Katika mashtaka hayo, Malinzi anakabiliwa na mashtaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za kimarekani 173,335 na Tsh 43,100,000.
Mwesigwa anakabiliwa na mashtaka sita ya kula njama ,kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji fedha.
Mshtakiwa Nsiande anakabiliwa na mashtaka mawili ya utakatishaji fedha, huku Zayumba akikabiliwa na mashtaka tisa ya kughushi na Frola anakabiliwa na shtaka moja la kughushi.
Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo walikana na upende wa mashtaka ukadai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wakaomba kuwasomea maelezo ya awali.
Katika maelezo hayo ya awali washtakiwa walikubali maelezo yao binafsi ikiwamo majina, nafasi zao za kazi na kuyakana maelezo mengine yote.
Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi May 14,17 na 21 ,2018 kwa ajili ya kusikilizwa.
Washtakiwa Zayumba na Flora walifanikiwa kupata masharti ya dhamana kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhamana kwa mujibu wa sheria.
Flora aliachiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini 2 ambao kila mmoja alisaini bondi ya Sh.mil 20, huku Zayumba akishindwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini 2 ambao watasaini bondi ya Sh.milion 100 kila mmoja.
Post A Comment: