Wataalam wa kufunga vifaa vya udhibiti na uhakiki wa vifaa vya mionzi kutoka Jumuiya ya Umoja wa Ulaya wameanza rasmi zoezi la kusimika mashine za kisasa kwenye jengo jipya la Maabara ya Tume Makao Makuu ya Ofisi za Atomiki jijini Arusha.
Wataalam hawa wamewasili nchini juzi tarehe 25/04/2018 tayari kwa kukamilisha zoezi hili ambalo pia linakwenda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wafanyakazi wa Tume jinsi ya kutumia vifaa hivyo kuboresha udhibiti wa matumizi salama ya mionzi maeneo mbalimbali nchini.
Zoezi linatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku 21 ambapo rasmi limeanza leo tarehe 27/04/2018 na kutegemewa kukamilika tarehe 17/05/2018.
Mashine ambazo zitafungwa ni kama ifuatavyo;
1.mashine moja ya Eksirei na mashine mbili Za Cobalt-60 na Caesium-137 kwa ajili ya kuhakiki vipimo vya mionzi.
2.Mashine ya kupima mionzi mwilini mwa binadamu au viumbe vingine ( Whole Body Counter)
3.Mashine ya kutayarisha sampuli za mazingira, mfano zenye urani (Fusion Machine).
Mashine hizi zitaifanya Tume iwe na vifaa vya kisasa vya kuhakiki vipimo vya mionzi.
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission) ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 7 ya mwaka 2003 baada ya kukoma kwa Sheria Na. 5 ya mwaka 1983 ambayo ilianzisha Tume ya Taifa ya Mionzi ( National Radiation Commission). Tume ina majukumu ya kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya mionzi.Tume ina jukumu la kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia na pia Kuishauri Serikali kuhusiana na mikataba ya Kimataifa kuhusu matumizi salama na uhamasishaji wa teknolojia ya nyuklia.
Imetolewa na;
Peter G. Ngamilo
Afisa Mawasiliano Mwandamizi
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania
S.L.P 743, Arusha, Tanzania
Simu/ Nukushi +255 27 29 70050/52/52/53
Barua pepe official@taec.or.tz
Website: www. taec.or.tz
Post A Comment: