Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi kanda ya Kaskazini Leo Komba amesema kuwa serikali itawachukulia hatua wamiliki wa ardhi wasiolipa kodi ya ardhi kwa mujibu wa sharia ya ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 hivyo amewataka kulipa kodi hiyo kwa wakati ili kuepuka kufikishwa mahakamani.

Akizungumza jijini Arusha Komba alisema kuwa wizara imejipanga kikamilifu kusimamia taratibu za kuwafikisha mahakamani wadaiwa wote watakaokaidi kulipa kodi ya ardhi na kukusanya kodi ya pango la ardhi kwa kila kipande cha ardhi kilichomilikishwa kwa mujibu wa sharia.

Aidha alisema kuwa Wizara imerahisisha ulipaji wa kodi ya pango la ardhi ambapo mmiliki akishapata Ankara ya madai anaweza kulipa kwa kutumia simu ya kiganjani .

“Pamoja na suala zima la ulipaji kodi la Ardhi ,Mhe.Waziri wa Ardhi ameanzisha kampeni ya Funguka kwa Waziri wa ardhi kuondoa migogoro ya ardhi ,Hivyo wale wananchi wenye kero za ardhi wanatakiwa kujaza fomu ambazo zipo kwenye ofisi zote za Halmashauri na Ofisi za wakuu wa Wilaya ili Waziri atatue kero hizo” Alisema Kamishna

Naye Afisa Ardhi Mwandamizi  Thadeus Riziki amesema kuwa ardhi ambazo hutozwa kodi hiyo ni zile ardhi ambazo zimepimwa na zina hatimiliki,maeneo ambayo hayajapimwa mengi hayajaingizwa katika mpango wa kulipa kodi.

Afisa huyo alisema kuwa serikali ina mpango wa kupima maeneo ambayo hayapimwa na pia kurasimisha makazi holela ili waweze kupatiwa huduma muhimu za kijamii.

Alisema kuwa ni vyema wananchi wakajijengea utaratibu wa kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu ikiwemo kufikishwa mahakamani .
Share To:

msumbanews

Post A Comment: