Mtu mmoja amefariki dunia na wawili kujeruhiwa baada ya kukatana kwa visu na mapanga katika ugomvi unaohusishwa na wivu wa mapenzi uliotokea katika Kitongoji cha Kirenero wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki alisema tukio hilo limetokea jana Aprili 17, 2018 asubuhi katika kitongoji cha Kirenero kijiji cha Kichongo wilayani Serengeti mkoani Mara.
Amemtaja aliyefariki kuwa ni Kibure Samwel (39) ambaye alichomwa kisu tumboni na kifuani wakati Nyang’anyi Waitara (44) mkazi wa Itununu, katika tukio hilo alikatwa mkono.
Munge Samwel (44) kaka wa marehemu alikatwa pajani na mtuhumiwa.
Amesema chanzo ni wivu wa mapenzi kwa kuwa mwanamke ambaye awali alikuwa mke wa Waitara kwa sasa ameolewa na Munge.
Kamanda huyo amesema tangu mwanamke huyo ambaye hakutajwa jina aolewe na Munge kumekuwa na mgogoro baina yao kuhusiana na hilo, na walipokutana inadaiwa walianza kushambuliana kwa maneno kisha kuanza kukatana.
“Aliyekufa ni mdogo wake na Munge Samwel ambaye katika ugomvi huo alifika kwenye tukio na kukuta kaka yake anashambuliana kwa silaha na Waitara, akaamua kuchukua panga kumsaidia ndipo mtuhumiwa akamchoma tumboni kisha kifuani na kufa papo hapo,”alisema.
Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Joseph Mwita alisema mgogoro huo ni wa muda mrefu ambapo Waitara alimshutumu Munge kuwa chanzo cha mgogoro wa ndoa yake mpaka mke akamfikisha mahakamani na kuomba talaka.
“Waitara (mtuhumiwa) aligoma kurudishiwa mahari na Munge ili amchukue mke wake kwa madai kuwa ameshazaa naye watoto watatu, hali iliyomlazimu Munge kumhamishia mwanamke huyo Tarime kwenye mji wake mwingine,” alibainisha.
Post A Comment: