Bei za simu za kisasa nchini zinatarajia kushuka baada ya Tanzania na China kuingia makubaliano ya ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza simu za mkononi hapa nchini.

Mbali na ujenzi wa kiwanda hicho, pia China itajenga kituo cha kutengeneza program za mawasiliano kwa ajili ya soko la Afrika na Mashariki ya Kati.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alitoa taarifa hiyo jana kupitia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Tweeter ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo; ambayo ilithibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga.

Aliitaja kampuni itakayotengeneza simu janja (smartphones) kuwa ni Shenzen-Qingchuan Technology (SQTL).

Licha ya kutokutaja lini uwekezaji huo utaanza na sehemu utakakofanyika, Balozi Kairuki alieleza kuwa ujio wa kiwanda hicho utafanya bei ya simu nchini, hususani simu janja kuwa nafuu.

"Kampuni hiyo imepanga kuwekeza nchini Tanzania kwa kujenga mtambo wa kutengeneza simu za mkononi pamoja na kituo cha kutengeneza simu za kisasa za mawasiliano kwa ajili ya soko la Afrika na Mashariki ya Kati," alisema balozi Kairuki.

Balozi Kairuki alisema kampuni hiyo ilieleza kuwa itazalisha simu zenye ubora na viwango vya soko la kimataifa.

Alieleza kuwa Kampuni hiyo pia imepanga kuajiri vijana 100 watakaopelekwa nchini China katika mji wa Shezen kupata mafunzo kwa muda wa miezi sita.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: