Na Veronica Kazimoto,Geita,
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imesajili jumla ya wafanyabiashara wapya 600
katika kampeni maalum ya utoaji huduma na elimu kwa mlipakodi
iliyofanyika mkoani Geita ikiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu masuala
mbalimbali ya kodi pamoja na kusikiliza malalamiko, changamoto na maoni
kutoka kwa wafanyabiashara hao.
Akizungumza
mara baada ya kukamilika kwa kampeni hiyo mwishoni mwa wiki, Menenja wa
TRA mkoani hapa James Jilala ameishukuru Idara ya Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi kwa kufika mkoani Geita hususani katika maeneo ambayo hakuna
ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na kufanikiwa kusajili
wafanyabiashara wengi ndani ya wiki moja.
"Nianze
kwa kuishukuru Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa hatua ambayo
mmeifanya ya kufika katika Mkoa wetu wa Geita hasa maeneo ambayo hatuna
ofisi ya TRA na kufanikiwa kusajili wafanyabiashara wengi kwa muda
mfupi kitu ambacho kimekuwa historia kwetu," alisema Jilala.
Jilala
alisema kuwa, baadhi ya wafanyabiashara walishindwa kusajiliwa na
kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa wakati, kwasababu
walitakiwa kusafiri zaidi ya kilomita 100 kwenda Geita mjini kwa ajili
ya kupata huduma hiyo. Hivyo, zoezi hili limewarahisishia wafayabiashara
kusajiliwa na kupatiwa TIN.
Naye
Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Gabriel
Mwangosi alisema kuwa , pamoja na usajili wa wafanyabiashara hao,
shughuli mbalimbali zimefanyika katika kampeni hiyo ikiwa ni pamoja na
utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali ya kodi
kupitia semina na kuwatembelea katika sehemu zao za biashara.
"Katika
zoezi hili tumefanya shughuli nyingi sana ikiwa ni pamoja na
kuwatembelea wafanyabiashara mahali wanapofanyia biashara zao,
tumesajili wafanyabiashara wapya na tumetoa semina mbalimbali ambazo
tunaamini kabisa zitakuwa zimebadilisha mtizamo, utendaji na mwenendo
mzima wa ulipaji kodi katika Mkoa huu wa Geita," alieleza Mwangosi.
Kampeni
ya huduma na elimu kwa mlipakodi ni moja ya mikakati ambayo Mamlaka ya
Mapato Tanzania imejiwekea katika kuhakikisha kuwa inasajili
wafanyabiashara 1,000,000 katika mwaka huu wa Fedha wa 2017/18.
Post A Comment: