Na Lydia Churi, Magreth Kinabo-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) ni taasisi ya Umma na siyo binafsi hivyo amekitaka kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kisheria kwa kushirikiana na Mahakama na kuacha kujiingiza kwenye masuala ya uanaharakati na siasa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam Jaji Mkuu amesema TLS ni chama huru cha kitaaluma kwa kuwa kilianzishwa kwa mujibu wa sheria kufanya kazi kwa manufaa mapana ya Umma.
“Hatuwezi kukubali chama hiki kikajisemea kuwa wao ni chama binafsi na tukakubali, dhana ya ubinafsi haipo”, alisisitiza Jaji Mkuu.
Alisema jukumu la TLS ni Kuisaidia Serikali na Mahakama kuhusu mambo yoyote yanayogusa sheria, utawala wa sheria na kazi za kisheria na akaongeza kuwa dhana hii ndiyo inayoiunganisha Taasisi hiyo na Mahakama ya Tanzania.
Aidha, Jaji Mkuu amewataka viongozi wa TLS kushirikiana na Mahakama pamoja na Mihimili mingine ya dola na kuacha malumbano kwenye vyombo vya habari kwa kuwa hayawasaidii kuendeleza chama hiki muhimu kwa wanasheria nchini.
Jaji Mkuu pia amewashauri viongozi wa chama hicho kumuheshimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwa Sheria na Kanuni zote ni lazima zipitie kwake.
Alisema Mamlaka ya Baraza la Uongozi la TLS katika Kutekeleza Majukumu ya Umma ni kusaidia kuboresha elimu ya sheria na taaluma ya Sheria Tanzania na kuwawezesha wanataaluma wa sheria kupata elimu ya ziada ya sheria kwa kadri mabadiliko yanayotokea nchini na duniani.
Majukumu mengine ya TLS ni pamoja na kuwawakilisha, kuwatetea na kuwasaidia wanasheria Tanzania kuhusu mazingira ya kufanya kazi za kisheria na kuwasaidia wananchi wa Tanzania katika masuala ya kisheria yanayogusa Sheria.
TLS ni Taasisi iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria za nchi kabla ya Uhuru na kukubalika kuendelea kuwepo kama Taasisi ya Kisheria kwa malengo ya kuanzishwa kwake kuelekezwa kwenye manufaa ya umma kwa kushirikiana na Mahakama, Bunge, pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Chama hiki kilianzishwa kwa Sheria ya Baraza la Kutunga Sheria (Legislative Council) Namba 30 ya 1954 na ni moja ya Sheria nyingi za iliyokuwa Tanganyika kabla ya Uhuru, ambazo kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Katiba ya Tanganyika ziliruhusiwa kuendelea kutumika Tanganyika ilipopata Uhuru Disemba 9 mwaka 1961 kama Sheria za Tanganyika huru.
Post A Comment: