SERIKALI imesema hakuna haja ya kubadilisha sheria ya uzazi iliyopo kwa sasa, sababu inampa fursa mwanamke kupumzika kutozaa mara kwa mara na kufuata uzazi wa mpango kama nchi inavyoelekeza na si vinginevyo.
Hayo yamesemwa Bungeni leo, Aprili 18 mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Sonia Juma Magogo, aliyetaka kufahamu mpango wa serikali wa kutaka kuwasaidia kina mama ambao wanajifungua kabla ya kipindi cha kuruhusiwa kupata miezi mitatu ya mapumziko ili waweze kuwanyonyesha vichanga na kuendelea majuKumu yao ya kazi.
“Kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2009, mtumishi wa umma anapojifungua hupewa likizo ya malipo ya siku 84, endapo atajifungua zaidi ya mtoto mmoja (mapacha) ataongezewa siku 14 na kuwa jumla ya siku 98.
“Lakini mtumishi akijifungua mtoto tena kabla ya kutimiza miaka mitatu, atapewa likizo maalum ya wiki sita ili kuhudumia mtoto wake kwa mujibu wa kanuni na baada ya hapo serikali inaweza kumuongezea siku za kupumzika kulingana na ushauri wa daktari.
“Ikumbukwe kwamba, likizo ya uzazi hutolewa mara moja katika kipindi cha miaka mitatu kwa kuzingatia sera ya afya ya mama na mtoto inayosisitiza kulinda na kujenga afya ya mama na mtoto na kuhimiza uzazi wa mpango. Sheria hizi ni za nchi nzima hivyo zinapaswa ziheshimiwe na kufuatwa kwa watumishi wa serikali na mashirika ya umma.
Aidha, Mbunge Mgila alisema uzazi wa mpango ni makubaliano ya wanandoa ikiwemo lini wazae na kuitaka serikali kubadilisha sheria hiyo ya likizo ambapo Waziri Mkuchika amesema kuzaa baada miaka mitatu inatosha huku akisema wanaume wawahurumie wanawake wanaowazalisha kila mwaka kwani nao wanahitaji kupumzika.
Mkuchika ametoa rai kwa watumishi wa umma au sekta binafsi, kuwa endapo yeyote atanyimwa haki ya likizo ya uzazi aitaarifu wizara husika ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya mwajiri wake.
Post A Comment: