Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imesema katika bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) mwaka 2017/18 kuna ongezeko la fedha lililotokana na gharama za kuhamisha watumishi wa ofisi hiyo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, kwamba ongezeko hilo ni zaidi ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge.
Akisoma taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa bajeti ya ofisi hiyo kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, mbunge wa Viti Maalum (CCM), Amina Mollel amesema katika mwaka wa fedha 2017/18 ofisi binafsi ya makamu wa rais ilitengewa Sh4.9bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Amesema hadi kufikia Februari 2018, ofisi hiyo ilipokea Sh5bilioni sawa na asilimia 103 ya bajeti ya matumizi ya kawaida, ikiwa ni ongezeko la asilimia tatu.
“Kiasi hicho kiliongezeka kutokana na gharama za kuhamisha watumishi wa ofisi ya makamu wa Rais kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma,” amesema.
Amebainisha kuwa pia ofisi hiyo mwaka 2017/18 ilitengewa Sh8.2bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, kwamba hadi kufikia Machi 2018 ofisi hiyo ilipokea Sh10.5bilioni sawa na asilimia 128 ya bajeti ya matumizi ya kawaida, ikiwa ni ongezeko la asilimia 28 zaidi ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge.
“Uchambuzi huu unaonyesha kumekuwa na mwenendo mzuri na wa kuridhisha kuhusu upatikanaji wa fedha kwa ofisi ya makamu wa rais. Maoni ya kamati ni kwamba hali hii ya upatikanaji wa fedha kwa wakati inatakiwa kuendelea na kuzingatiwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19,” amesema Mollel.
Post A Comment: