Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imesema hadi kufikia Juni 30 mwaka huu inatarajia kuajiri walimu 6,000 wa masomo ya Hisabati na Sayansi kwa ajili ya shule za sekondari nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali, ambaye alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuondoa changamoto katika shule za kata ikiwamo upunguzu wa walimu wa Hisabati na Sayansi.

Pia, Bobali alitaka kujua msimamo wa serikali kuhusu wananchi kuchangia kwenye chakula ambacho wameona ndio chachu ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika Mkoa wa Lindi. Alisema hadi Desemba mwaka 2017, Serikali ilikuwa imeajiri walimu 200 wa Hisabati na Sayansi kwa ajili ya shule za sekondari.

Kadhalika, alisema serikali haijazuia wananchi kuchangia maendeleo ya shule walichokataza ni kumzuia kumpa adha ya kukosa masomo mwanafunzi ambaye ameshindwa kuchangia michango hiyo.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua kama serikali imefanya tathmini juu ya ubora na changamoto zilizopo katika shule za sekondari za kata nchini.

Akijibu Kakunda alisema hadi Oktoba 2017, Shule za kata 3,103 zilikuwa na wanafunzi 197,663 ambao kama zisinge kuwepo wangeikosa elimu ya sekondari.

Kakunda alisema maamuzi ya kuanzishwa kwa shule ya sekondari kila kata ili kuhakikisha watoto wengi zaidi waliokuwa wanakosa nafasi za masomo ya sekondari licha ya kufaulu mitihani ya darasa la saba kwa sababu tu ya uchache wa shule wanapata nafasi hizo.

Alisema tathmini mbili za serikali zilizochambua kwa kina sekta ya Elimu kupitia Tume ya Prof. Mchome ya mwaka 2013, iliyochambua sababu za ufaulu hafifu wa wanafunzi kwenye mitihani ya mwaka 2012 na kamati ya kuhuisha na kuoanisha sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya mwaka 1996.

Pia alisema sera ya Taifa ya Elimu ya juu ya mwaka 1999 na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa elimu ya msingi ya mwaka 2007, iliyoongozwa na Mwalimu Abubakar Rajab mwaka 2013, ndizo zilizobaini na kuishauri serikali kuanzisha sera mpya moja ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.

“Sera mpya imetoa maelekezo mahususi kuhusu namna ya kuboresha elimu ya awali, msingi, sekondari, elimu ya ufundi na elimu ya juu na mitaala imesharekebishwa, ikama, vifaa, samani na miundombinu vyote vinaendelea kuboreshwa,” alisema.
Share To:

msumbanews

Post A Comment:

KARIBU WINNING SPIRIT PRE & PRIMARY SCHOOL ARUSHA

Winning Spirit Pre & Primary School Inawatangazia wazazi/Walezi wote wenye watoto waliofikia umri wa kuanza shule ya awali kuanzia miaka miwili na...

Jan 13 2025 - MsumbaNews Blog