Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Ndugu Wallace Karia ametuma salamu za pongezi kwa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17(Serengeti Boys) kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Vijana kwa nchi za Africa Mashariki na kati Cecafa mashindano yaliyofanyika nchini Burundi.

Serengeti Boys wametwaa ubingwa huo wa Cecafa baada ya kuifunga Somalia katika mchezo wa fainali iliyochezwa Uwanja wa Ngozi kwa mabao ya EdsonJeremiah na Jaffar Juma Mtoo.

Rais wa TFF Ndugu Karia aliyekuwa nchini Burundi amesema Vijana hao waliocheza kwa kujituma mwanzo wa mashindano mpaka fainali wameiletea sifa kubwa Tanzania na ni jambo la kujivunia kwa kila Mtanzania.

Amesema ushindi huo unatoa picha nzuri ya muelekeo wa mpira wa Tanzania kupitia soka la vijana.

“Vijana wetu wameonesha soka zuri na wamefanya kazi nzuri sana katika mashindano ya Cecafa ,kwa niaba ya TFF nawapongeza vijana wetu na benchi la ufundi ambalo pia limefanya kazi nzuri kuhakikisha vijana wanafanya vyema,tutaendelea na jitihada zetu za kuendelea kuwekeza kwenye soka la vijana ambalo ndilo msingi” amesema Rais wa TFF Ndugu Karia.

Amesema timu hiyo ya Serengeti Boys iliyokwenda Burundi ndio inayoandaliwa kwa fainali za vijana za Africa chini ya miaka 17 ambazo Tanzania itakua mwenyeji wa fainali hizo zitakazofanyika mwakani.

Ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na TFF katika kuendeleza mpira na kushirikiana kwa karibu na uongozi wa TFF uliopo madarakani.

Pia amewashukuru WaTanzania kwa kuendelea kuziunga mkono timu za Taifa ikiwemo Serengeti Boys na kuwaomba kujitokeza kwa wingi kuwapokea vijana hao watakaporudi kutoka nchini Burundi.

Serengeti Boys wanatarajia kutua nchini Jumatano Saa 8 usiku kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA).
Katika mashindano hayo Serengeti Boys ilitoka sare 1-1 na Uganda kabla ya kuifunga Sudan 6-0 na baadaye kuichapa Kenya kwa mabao 2-1 kwenye nusu fainali na kushinda mabao 2-0 dhidi ya Somalia kwenye mchezo wa fainali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: