Rais wa zamani wa Malawi, Dkt. Joyce Banda anatarajia kuingia nchini humo wiki hii baada ya kuishi miaka minne uhamishoni.
Dkt. Banda aliondoka nchini humo baada ya jeshi la polisi kutoa amri ya kumkamata akidaiwa kujihusisha na rushwa.
Msemaji wa Banda, Nowa Chimpeni amesema kuwa chama chake cha People’s Party (PP) kinampokea akiwa na lengo la kukijenga upya katika kuelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2019.
“Naweza kuthibitisha kwa wafuasi na wananchi wa Malawi kwamba rais wa zamani wa nchi hii, Dkt. Joyce Banda atawasili Jumamosi ya wiki hii,” alisema Chimpeni na kuongeza kuwa Banda atakiunga upya chama chake baada ya viongozi wengi kuondoka wakitimkia kwenye chama cha Democratic Progressive Party (DPP).
Dkt. Banda amekuwa akitembelea nchi za Uingereza, Afrika Kusini pamoja na Marekani katika kipindi cha miaka minne, akiwa uhamishoni.
Msemaji wa Jeshi la polisi, James Kadadzera amesema kuwa hati ya kumkamata bado inaendelea kuwepo lakini alikataa kueleza kama Dkt Banda anaweza kukamatwa punde atakapoingia nchini humo.
Post A Comment: