Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza madaktari na wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Jijini Dar es Salaam kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo.

Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ametoa pongezi hizo hizo tarehe 18 Aprili, 2018 alipotembelea taasisi hiyo na kuwajulia hali wagonjwa wanaopatiwa matibabu akiwemo Waziri Mstaafu Dkt. Juma Ngasongwa.

Mhe. Rais Magufuli amesema JKCI ambayo imepata mafanikio katika matibabu ya moyo kwa njia ya upasuaji wa tundu dogo na kufungua kifua imesaidia kuokoa vifo kwa Watanzania wengi waliokuwa wanakosa uwezo wa kifedha wa kwenda kutibiwa nje ya nchi, imepunguza gharama za kutibiwa nje ya nchi na imeijengea heshima Tanzania.

“Prof. Janabi, madaktari wote na wauguzi wa taasisi hii nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya, natambua kuwa wapo baadhi ya waliokuwa wananufaika na wagonjwa kupelekwa nje ya nchi hawatafurahia kazi mnayoifanya lakini nyinyi chapeni kazi na Serikali ipo na nyinyi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuitembelea taasisi hiyo na kuwatia moyo na ameahidi kuwa wataendelea kuchapa kazi kwa juhudi ili kuimarisha zaidi huduma za matibabu ya moyo.

Amefafanua kuwa JKCI imefanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wanakwenda kutibiwa nje ya nchi kwa asilimia 83 na kwamba tangu mwaka 2015 idadi ya wagonjwa waliotibiwa katika taasisi hiyo ni zaidi ya 2,420 ambao wangehitaji wastani wa Shilingi Milioni 30 kwa kila mmoja kutibiwa nje ya nchi.

Kabla ya kutembelea JKCI Mhe. Rais Magufuli na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli wamekwenda Kariakoo Jijini hapa kutoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo ambaye amefiwa na Mama yake Bi Rehema Paulo Mombuli, ambaye mwili wake unasafirishwa kwenda Arusha na baadaye Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Share To:

msumbanews

Post A Comment: