Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutilia mkazo ajenda zitakazoimarisha zaidi umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano baina ya nchi wanachama ili kufanikisha jukumu muhimu la kupambana na umasikini wa wananchi na kukuza uchumi.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 24 Aprili, 2018 wakati akihutubia Bunge la Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani, katika ukumbi wa Pius Msekwa uliopo ndani ya viwanja vya Bunge Mjini Dodoma ambako Bunge hilo linafanyia vikao vyake kwa mara ya kwanza katika mji huo.

Mhe. Rais Magufuli amesema Wabunge hao wanao wajibu wa kushughulikia migogoro ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya wananchi, vikwazo vya biashara na uwekezaji, na kutilia mkazo ujenzi wa viwanda vitakavyochakata na kuzalisha bidhaa zitokanazo na rasilimali lukuki zilizopo ndani ya Afrika Mashariki ili manufaa ya rasilimali hizo yawanufaishe wananchi.

Ametaja miongoni mwa mambo yanayopaswa kutiliwa mkazo na nchi zote kuwa ni kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na uzalishaji wa umeme wakutosha na wenye gharama nafuu, ambavyo ni muhimu katika ujenzi wa viwanda.

“Tafiti zinaonesha gharama za usafiri kwenye ukanda wetu ni mara 4 hadi 5 ukilinganisha na gharama za Asia Mashariki, Marekani na Ulaya na zinachangia kuongezeka kwa gharama za bidhaa kwa asilimia 40.

“Umeme pia umeonekana kuwa sio mwingi, utafiti uliofanywa na taasisi ya Power Africa mwaka 2015 umeonesha kuwa nchi zote 6 za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina takribani megawati 6,500 tu za umeme, hiki ni kiwango kidogo mno kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa kisasa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Katika kutekeleza azma hiyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza na kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo, na pia ameshauri nchi wanachama zisitegemee misaada pekee na badala yake zifikirie kutekeleza miradi kwa fedha zake zenyewe ili kuokoa muda na kupunguza gharama za miradi husika.

Mhe. Rais Magufuli amezungumzia juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kufikia dhamira hiyo kuwa ni pamoja na kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo itaunganisha hadi nchi za Burundi, Rwanda na Uganda, kujenga meli katika ziwa Victoria, kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), kununua ndege 6, kujenga barabara, kupanua bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, kuboresha viwanja vya ndege 11 na amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na nchi nyingine wanachama wa Afrika Mashariki.

“Nataka kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Afrika Mashariki kuwa Serikali ninayoiongoza itaendelea kushirikiana na Bunge hili katika masuala mbalimbali ya kuiunganisha jumuiya yetu, na ninawaomba nanyi mtekeleze wajibu wenu wa kuwaunganisha na kuwaelimisha wananchi ili waone umuhimu wa jumuiya hii” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Martin Ngoga amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kulihutubia Bunge hilo na amempongeza kwa jitihada zake za kujenga nidhamu ya utumishi wa umma, kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kukuza uwekezaji na biashara ikiwemo ujenzi wa viwanda na kuonesha uongozi mahiri, na ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono juhudi hizo.

Pamoja na Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, viongozi wengine waliohudhuria wakati Mhe. Rais Magufuli akihutubia bunge hilo ni Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu wa Pili wa Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Kirunda Kivejinja, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri, Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
24 Aprili, 2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: