Rais John Magufuli amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isaac Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge kufuatilia ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji katika Mkoa wa Dodoma na kuhakikisha wahusika wanakamatwa au maji yanatoka.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Aprili 27, wilayani Kondoa wakati wa hafla ya uzinduzi wa barabara ya Dodoma – Babati yenye urefu wa kilomita 251 ambayo ni sehemu ya barabara kuu inayotoka Capetown, Afrika Kusini mpaka Cairo, Misri.

Ameagiza vyombo vya dola kuwatafuta wahusika wa ubadhirifu wa fedha hizo ambazo amesema ni zaidi ya Sh2 bilioni.

Amesema ni lazima wahusika wachukuliwe hatua kwa sababu hizo ni fedha za wananchi, na ni vyema ziwaletee maendeleo.

“Haiwezekani tukawa tunaimba maji kila siku halafu maji hayatoki. Vyombo vya dola vihakikishe wahusika wote wanakamatwa au maji yanatoka. Tukibembelezana hivi hatutafika, hata hii barabara tusingebana, isingekamilika,” amesema Rais Magufuli.

Awali kabla ya Rais Magufuli kuzungumza, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema kuna ubadhirifu wa Sh1.5 bilioni kwenye mradi wa maji katika wilaya za Kondoa na Chemba ambao mpaka sasa  unasuasa.

Mkuu huyo wa mkoa alisema mradi huo ulitengewa  Sh2.8 bilioni kwa ajili ya wilaya hizo, lakini kulitokea ubadhirifu wa Sh1.5 bilioni.

Amebainisha kwamba vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wa ubadhirifu huo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: