Ndoa ya mwanamuziki Alikiba na mchumba wake Amina inatarajiwa kufungwa Leo alfajiri katika msikiti wa Ummul Kulthum ulioko eneo la Kizingo jijini Mombasa.
Mama wa bibi harusi mtarajiwa, Bi Asma Said anasema ndoa hiyo itafungwa katika msikiti huo uliojengwa na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho.
Anasema baada ya ndoa kufungwa itafuatiwa na sherehe ya kupambwa bibi harusi ambayo itafanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini humo.
Miongoni mwa watu mashuhuri wanaotarajiwa kuhudhuria harusi hiyo ni Rais wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete na Ommy Dimpoz.
Bi Asma anasema maandalizi yanaendelea vizuri na nyumbani kwa bibi harusi mwandishi alishuhudia wanawake wakiwa wanajipamba huku wengine wakijipaka henna.
Alibainisha kuwa tayari bwana harusi ameingia nchini Kenya huku wadokezi wakisema kuwa Alikiba alikuwa katika hoteli ya English Point Marina ambapo ni karibu na nyumba ya bibi harusi iliopo eneo la Kongowea.
“Kijana ametoka Tanzania na kuja kuoa Kenya mimi sikujua kama mtoto wangu ataolewa na Alikiba lakini Mungu ndio aliyepanga,” akasema Bi Asma
Post A Comment: