BUNGE limeelezwa kuwa Jeshi la Polisi halina muda wa kulinda taasisi au chombo chochote kitakachotaka kufanya mikutano au maandamano yasiyo na tija.
Aidha, amesema hakuna idadi kubwa ya kutosha kwa askari polisi wa kulinda mikutano ya vyama vya siasa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mkoani (CUF), Twahir Awesu Mohamed.
Katika swali lake, mbunge huyo alihoji ni kwa nini polisi waliwalinda wanachama wa CCM waliofanya maandamano makubwa hivi karibuni visiwani Zanzibar.
Katika swali lake, mbunge huyo alihoji ni kwa nini polisi waliwalinda wanachama wa CCM waliofanya maandamano makubwa hivi karibuni visiwani Zanzibar.
“Kumekuwa na katazo la kufanya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa lakini Aprili 8, mwaka huu, CCM mikoa miwili ya Pemba waliandamana chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi wakiwa wamebeba mabango wakiimba nyimbo za kuhalalisha amani na uchochezi. Hili katazo linahusu vyama vya upinzani pekee au vyama vyote?” alihoji.
Aidha katika swali la msingi, mbunge huyo alihoji ni lini jeshi la polisi litafanya kazi zake kisayansi zaidi na kuondokana na kutumia nguvu zisizo za lazima wakati wa kutekeleza majukumu yake
“Suala la weledi kwa watendaji wa polisi linasimamiwa vipi ili polisi waweze kupambana na uhalifu unaokuwa kitaalam kila siku,”alihoji.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Masauni alisema suala la kuandamana kama yameruhusiwa lazima jeshi la polisi litoe ulinzi.
“Kipindi hicho ambacho serikali ina shughuli nyingi za kiuchumi, jeshi la polisi haliwezi kuendekeza kutoa ulinzi katika maandamano au mikutano kwa kuwa hatuna askari wa kutosha wa kufanya shughuli hizo,”alisema.
Alisema kwa taasisi au chombo chochote kitakachohitaji kufanya maandamano au mikutano jeshi la polisi halina muda huo.
Alisisitiza kuwa sheria ni msumeno inakata kote kote hivyo ni vyema sheria zikafuatwa.
Alifafanua kuwa katika kutekeleza kazi zake polisi anaruhusiwa kutumia nguvu inayoendana na mazingira ya tukio
Aidha alisema serikali imekuwa ikiwajengea uwezo wa kiutendaji askari kwa kutoa mafunzo mbalimbali sehemu za kazi yenye lengo la kuwakumbusha taratibu za kazi.
Alifafanua kuwa katika kuhakikisha linafanya kazi kwa weledi jeshi la polisi limekuwa likiajiri wasomi wenye taaluma mbalimbali kama vile teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), maabara, uchunguzi wa nyaraka na taaluma zingine zinazohusisna na makosa yanayosababishwa na ukuaji wa teknolojia.
Post A Comment: