Mke wa mwigizaji na mchekeshaji maarufu nchini, Amri Athumani ‘Mzee Majuto’, Aisha Yusufu (39), amewaomba Watanzania wamuombee mume wake apone na aendelee na shughuli zake.

Mzee Majuto ambaye alifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Tumaini jijini Dar es Salaam, Januari mwaka huu na kuruhusiwa, alirudishwa tena hapo jana baada ya hali yake kuwa mbaya kutokana na kidonda kushindwa kufunga.

Aisha amesema mume wake alifikishwa hapo akiwa katika hali mbaya lakini anashukuru kwa sasa anaendelea vizuri.

“Ninachoomba Watanzania waendelee kumuombea tu mume wangu apone na kuruhusiwa kutoka hospitali kwa kuwa akilala kitandani na mambo yake yanalala,” amesema.

Amesema huo ni upasuaji wa pili kwa Majuto kufanyiwa baada ya ule wa kwanza wa henia aliofanyiwa jijini Tanga  Julai mwaka jana.

“Wakati tunahangaika kuangalia namna ya kupata tiba ya nyonga ndipo alipogundulika kuwa ana tezi dume na hivyo kufanyiwa upasuaji,” amesema.

Mzee Majuto amewahi kucheza filamu mbalimbali ikiwemo Welcome Back, Mshamba, Pedeshee, Si Sawa, Mama Ntilie, Nahama, Gumzo, Mrithi Wangu, Rent House, Ndoa ya Utata, Daladala na Nimekuchoka.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: