Mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbali mbali nchini zimeendelea kuleta madhara mkoani Rukwa, ambapo zimesababisha uharibifu wa mashamba ya vyakula na kuharibu mazao.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoani Rukwa, George Kyando ambapo amesema kuwa mvua hizo zimezoa mazao kwenye mashamba mkoani humo na mengine kuyafunika kwa udongo, hali ambayo imeleta hasara kwa wakulima.

Kamanda Kyando amesema kuwa barabara mbalimbali zimekatika na kukosa mawasiliano, huku baadhi ya madaraja yakizolewa na maji lakini hakuna taarifa ya vifo waliyoipata mpaka sasa.

“Huku Rukwa kuna barabara inayopita bonde kwa bonde kutoka mkoa wa Rukwa kwenda Katavi, kutokana na hizi mvua zinazonyesha madaraja yamechukuliwa na maji, barabara zimekatika, mashamba ya mipunga na mahindi yamefunikwa na udongo, kwa hiyo tumepata hayo majanga lakini tunashukuru Mungu hakuna mtu yeyote ambaye amedhurika na hiyo mvua, ni miundombinu na mashamba tu,”amesema Kyando

Hata hivyo, kutokana na mvua hizo Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania imewataka wananchi kuwa makini wanaposafiri na kutembea, kwani mvua kubwa zaidi inatarajiwa kunyesha siku za hivi karibuni.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: