Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma amefunguka na kuweka wazi sababu kubwa iliyopelekea yeye kukamatwa nchini China na kusema chanzo kilikuwa kutaka kupigana ngumi na mwenzake jambo ambalo lilipelekea kulipa zaidi ya milioni kumi ya Kitanzania.
Msukuma amesema hayo bungeni wakati akichangia bungeni ambapo amemuomba Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi alete mapendekezo bungeni ili waweze kufanya marekebisho ya sheria kuwawezesha baadhi ya mahabusu ambao wana makosa madogo kuachiwa ili kupunguza msongamano magereza pamoja na mahakama kwa kudai kuwa saizi mahakama pamoja na magereza zimejaa mahabusu tu.
Mbunge Msukuma ametolea mfano gereza la Geita ambalo kwa uhalisia wake amedai linauwezo wa kuchukua watu 141 lakini mpaka juzi April 18, 2018 lilikuwa na watu zaidi ya 750 na kusema hiyo ni hali mbaya huku akidai wengi ni mahabusu wenye makosa madogo madogo.
"Mimi nakumbuka siku moja nilikuwa Hong Kong nchini China nilifanya kosa yaani tulikuwa tu tunabishana na kutaka kupigana ngumi na huyo mwenzangu lakini nilipoitiwa polisi walikuja kuniomba tu kitambulisho changu pekee yake na nilipowapa kitambulisho wakaniachia ila sasa siku ambayo tulikuwa tunataka kutoka tulitozwa faini ya dola elfu tano palepale uhamiaji wakati wa kugongewa 'passport' sasa Tanzania mtu akisema tu huyu kanitukana, huyu amenidhulumu hata mtu hajahakikisha wanaenda kumuweka magereza" alisema Msukuma
Mbunge Msukuma amemtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi kufanyia kazi mambo madogo madogo hayo katika wizara yake hususani katika mahakama na magereza ili aweze kuyarekebisha.
Post A Comment: