Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga amesema ndege aina ya Airbus 380, EK701 ya Shirika la Ndege ya Emirates si ya kwanza yenye ukubwa huo kutua nchini kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Akizungumza  leo Aprili 25 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2018/19, Mlinga amesema ndege ya kwanza kubwa kutua nchini ni aina ya Antonov mwaka 2009 ikiwa imepakia mitambo ya kufua umeme ya Richmond.

“Iliyokuja kipindi kile (Antonov) ilikuwa na uzito tani 285 wakati hii iliyokuja jana ina tani 276. Iliyokuja kipindi kile ilikuwa na injini sita, ila hii iliyotua jana ina injini nne. Ndege hii iliyoleta mitambo ya Richmond ilikuwa na  urefu wa mita 88 ila hii ya jana ina mita 73,” amesema Mlinga.

Ndege hiyo ya shirika la Emirates iliyokuwa ikielekea Mauritius  ilitua jana kwa dharura katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kutokana na hali mbaya ya hewa nchini humo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari alisema ni mara ya kwanza kwa ndege yenye ukubwa huo aina ya ‘Airbus’ kutua katika ardhi ya Tanzania.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: