MBEYA City imesema haikubaliani na namna ambavyo mchezo wao dhidi ya Yanga ulivyochezeshwa jijini hapa hivi karibuni na hivyo wanakata rufaa kupinga upatikanaji wa bao la Yanga kwa kuwa haikuwa rafu.
Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe amesisitiza mjini hapa kwamba wamekasirishwa na maamuzi mabovu ya mwamuzi Shomary Lawi ambaye alionekana kushindwa kuumudu mchezo huo uliokumbwa na vurugu za ndani na nje ya uwanja.
Kimbe alidai kuwa hiyo ni mara ya pili kwa mwamuzi huyo kutoa maamuzi mabovu huku akikumbushia mchezo wa mzunguko wa kwanza kati ya Mbeya City dhidi ya Stand United uliyochezwa mwaka jana mkoani Shinyanga.
“Tunakata rufaa kupinga maamuzi mabovu ambayo yalitolewa kwenye mchezo wetu dhidi ya Yanga ,faulo ile ambayo ilizaa bao la Yanga haikuwa halali lakini pia tunatoa malalamiko yetu juu ya faulo ambayo aliicheza Chirwa dhidi ya Ramadhan Malima,” alisema Kimbe.
Pia Kimbe alizungumzia sakata la mchezaji Eliud Ambokile ambaye alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Danny Joram mnamo dakika ya 96 kisha baadae kuingia tena.
“Eliud Ambokile ni kweli alifanyiwa mabadiliko lakini wakati yanafanyika alikuwa hajui kuwa nafasi yake imechukuliwa na mtu mwingine ,lakini cha ajabu mwamuzi namba mbili alimuuliza Eliud kama anaweza kuendelea na baadae Eliud akaruhusiwa kuingia,”alisema kiongozi huyo ambaye amehusika na mikataba yote ya udhamini wa Mbeya City.
“Wakati Eliud anarudi uwanjani mwalimu Ramadhani Nsanzurwimo aliinuka na kumfuata mwamuzi wa mezani kumtaka amjulishe mwamuzi kuwa kuna mtu ameingia wakati akiwa amefanyiwa mabadiliko na ndipo viongozi wa Yanga nao wakamfuata mwamuzi na kuanza kumlalamikia,” alisema Kimbe.
Mbeya City wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Singida United utakaochezwa siku ya Ijumaa.
Post A Comment: