Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un ametangaza kusitisha majaribio ya makombora ya nyuklia kuanzia leo, ikiwa ni hatua ya kutengeneza mazingira bora zaidi ya mazungumzo kati yake na Korea Kusini.
Uamuzi huo wa Kim Jong-un umetangazwa na Shirika la Habari la Kikorea (KCNA). Kwa mujibu wa taarifa hizo, Kiongozi huyo amesitisha majaribio hayo ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano mkubwa wa mazungumzo kati yake na viongozi wa Korea Kusini yenye lengo la kutatua mgogoro wa kinyuklia katika eneo hilo.
KCNA imeeleza kuwa Pyongyang inaweza kufunga kabisa vituo vyake vya utengenezaji wa mabomu hayo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uchumi wake na kutafuta amani katika eneo hilo.
“Hatuhitaji tena mpango wowote wa kufanya majaribio ya makombora ya nyuklia yanayoishia katika eneo hili au yanayovuka bara, na kwa sababu hiyo vituo vya kutayarisha makombora hayo vya kaskazini vimemaliza mpango wake,” KCNA imemkariri Kim Jong-un.
Kwa mujibu wa KCNA, Korea Kaskazini imeahidi kuunga mkono juhudi za kimataifa za usitishwaji wa majaribio ya nyuklia na kwamba haitatumia silaha za kinyuklia kwakuwa hakuna tishio tena dhidi ya nchi hiyo.
Kiongozi huyo pia anajiandaa kukutana kwa mara ya kwanza na rais wa Marekani, Donald Trump katika juhudi za kutafuta suluhu ya mgogoro wa kinyuklia kati ya nchi hizo na washirika wao.
Post A Comment: