KATIKA kupunguza presha ya mechi ya watani wa jadi Yanga, Kocha Mkuu wa Simba Mfaransa, Pierre Lechantre amezuia kambi ya moja ya hoteli kubwa ya nyota tano iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Kambi hiyo ilikuwa ya maandalizi ya mechi ya watani wa jadi wa Simba na Yanga iliyotarajiwa kupigwa jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kocha huyo alizuia kambi hiyo ya hoteli kubwa baada ya uongozi wa timu hiyo kupendekeza kuipeleka huko kabla ya kwenda kwenye hoteli yao wanayokaa kila mara iliyopo Mbezi Beach.
Mtoa taarifa huyo alisema, kikubwa kocha huyo alitaka wachezaji wake waione mechi hiyo ya kawaida kama zilivyo mechi nyingine walizocheza awali.
“Uongozi wetu ulipanga timu ifikie kwenye moja ya hoteli kubwa ya nyota tano (jina tunalo tunalihifadhi) wakati timu inatoka Morogoro ilipoweka kambi ya mechi dhidi ya Yanga.
“Lakini tulipomtaarifu kocha, alikataa kabisa na kuuomba uongozi kuiweka timu kwenye kambi yao waliyoizoea ambayo kila siku tumekuwa tukiweka kwa ajili ya maandalizi.
“Na kikubwa kocha alitaka kuwaweka sawa kisaikolojia kwa kuwataka waione ni mechi ya kawaida kwa maana timu ukiiweka kambini kwenye hoteli kubwa kutawafanya wachezaji wacheze kwa presha kubwa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa kocha huyo kuzungumzia hilo alisema: “Ninataka wachezaji wangu waione mechi hii kuwa ya kawaida tofauti na mashabiki wanavyofikiria.
“Kwa sababu kama timu ukiweka kambi kwenye hoteli kubwa wataiona mechi kubwa na presha kuongezeka kitu ambacho sikukitaka na ndiyo maana nimependekeza tufikie kwenye hoteli hiyo tuliyoizoea.”
Post A Comment: