WAZIRI
wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala ametuma salamu kwa
majangilli wanaojihusisha na uwindaji haramu wa wanyama kwenye Hifadhi
za Taifa ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Amesema
Serikali na wadau wengine wamejipanga kuhakikisha rasilimali za nchi
zinalindwa kwa kudhibiti ujangili wa wanyama na viumbe hai vyote
vinavyotokana na maliasili yetu ya asili kwenye hifadhi za Taifa.
Dkt.
Kigwangala alituma salamu hizo kupitia Mbio za Ngorongoro Marathon
zilizofanyika jana Aprili 21, 2018 kwa kuanzia Lango Kuu la kuingilia
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuishia Uwanja wa Mazingira Bora
mjini Karatu mkoani Arusha.
Pamoja
na kuwa mgeni rasmi kwenye mbio hizo, Dkt. Kigwangala pia alikimbia
kilomita 21 kuanzia saa 3.30 asubuhi na kumaliza saa 6.20 mchana, na
kusema hiyo ni ishara tosha ya kujipanga na kukabiliana na majangili.
Dkt.
Kigwangala alisema kwa kumaliza mbio hizo, sio tu anawatishia majangili
kuwa yupo vizuri kukabiliana nao, bali anataka askari wote wa wanyama
pole wawe wakakamavu na asimuone askari yeyote mwenye kitambi.
“Moja
ya malengo ya mbio za Ngorongoro Marathon kwa mwaka huu ni kupambana na
ujangili na majangili. Na sikumaliza mbio hizi za kilomita 21 kwa
bahati mbaya, bali ni kuwadhihirishia majangili na watu wote wenye nia
mbaya na rasilimali zetu kuwa nipo fiti.
“Lakini
sio kwa majangili, hata kwa askari wetu, nataka kuwaeleza kuwa kuanzia
sasa sitaki kuona askari anakuwa na kitambi. Hatuwezi kupambana na
majangili kama askari wetu wana vitambi na wapo legelege… Na nataka
kuwaeleza askari kama wanataka twende nao pamoja kwenye hili basi
wajipange” alisema Kigwangala.
Dkt.
Kigwangala alisema nia nyingine ya NCAA kudhamini mbio hizo ni
kutangaza shughuli za utalii ndani na nje ya nchi, kwani anaamini
kupitia waandishi wa habari na washiriki wa mashindano hayo kutokea
ndani na nje ya nchi, itawezesha kuongeza watalii na hifadhi hiyo
kujulikana zaidi.
Naye
Rais wa Chama cha Riadha nchini (RT) Anthony Mtaka, alisema moja ya
mambo yanayotushinda nchini ni kujitangaza, lakini hapo hapo kushindwa
kupenda vya kwetu, kwani pamoja na kuwa Mlima Kilimanjaro upo Tanzania,
lakini matangazo yake mengi yapo Kenya.
Mtaka
ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alisema amefurahishwa na uongozi
wa NCAA kudhamini mashindano hayo, kwani yatawezesha Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro kufahamika duniani kote.
“Kwenye
Serikali ukiwa na mtu kama Dkt. Fred Manongi (Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro) mambo yatakwenda vizuri. Tumempa taarifa wiki
mbili kabla ya mashindano kumuomba atudhamini, lakini akawa amekubali na
mambo yamekwenda vizuri.
“Hiki
cha kukubali kudhamini mashindano haya ni kikubwa sana. Sasa anatufanya
Watanzania tuanze kujitangaza na kupenda vya kwetu. Hili tatizo la
kushindwa kujitangaza ni kubwa ndiyo maana kila siku kuna malalamiko
kuwa Kenya wanajitangaza Mlima Kilimanjaro ni wa kwao. Sisi sasa tujitoe
na kuonesha rasilimali hizi za utalii ni za kwetu” alisema Mtaka.
Post A Comment: