Wakati
polisi wakitoa tahadhari kwa wananchi kuhusu maandamano yaliyoratibiwa
kwenye mitandao ya kijamii na kupangwa kufanyika leo, Balozi wa Tanzania
nchini Sweden, Dk Wilbrod Slaa amesema ofisi yake ilipokea barua kutoka
polisi wa nchi hiyo kuhusu taarifa za Watanzania waliotaka kuandamana
jana.
Hata hivyo, hapa nchini polisi imeonya ikisema maandamano hayo ni batili na atakayeshiriki atashughulikiwa.
Akizungumza
na gazeti la Mwananchi kutoka nchini Sweden, Dk Slaa alisema jana kuwa,
polisi walisema wameshawapa kibali waandamanaji na watawapa ulinzi
unaostahili.
“Ilipofika
saa tatu asubuhi, walifika watu kumi, polisi hawakuwa na kazi kubwa
waliwapangia wapi wasimame, walikuja na mabango yao. Lakini hakukuwa na
muziki kwa sababu huku hawatakiwi kupiga muziki,” alisema.
Alisema
baada ya kuwaona waandamanaji hao wakiwa na mabango yenye ujumbe
mbalimbali, walikubaliana na polisi kuwa waingie ndani ili kujua nini
wanachohitaji.
“Walikataa
kuingia ndani na kusema hawana sababu ya kujadiliana. Tukawaambia
tunawaomba watu viongozi wawili ili wawe wawakilishi na viongozi hao
waseme nini wanachotaka, lakini pia walikataa,” alisema.
Dk
Slaa alisema Sweden ni moja ya nchi zenye vyama vya Watanzania
vilivyosajiliwa kuanzia ngazi ya mkoa na kuendelea na viongozi wa vyama
hivyo walipiga simu ubalozini wakimsifu Rais Magufuli.
“Nimepokea
simu kutoka sehemu mbalimbali, kwamba wanamuunga mkono Rais John
Magufuli. Wanataka Rais asilegeze kamba katika vita dhidi ya rushwa na
matumizi mabaya ya mali za umma kwa sababu vita hivyo vinatengeneza
maadui ndiyo maana mambo kama haya
yanatokea,” alisema.
Kuhusu
ujumbe aliosema ni wa upotoshaji ulioandikwa kwenye mabango ya
waandamanaji hao, Balozi Slaa alisema unamhukumu Rais kwa mambo ambayo
mahakama haijathibitisha.
Chanzo; Mwananchi
Post A Comment: