Serikali
imesema kanuni mpya za maudhui kwenye mitandao, runinga na redio
zimetungwa kwa lengo la kudhibiti usambazaji wa kauli chafu, matusi,
picha za utupu na zenye maudhui yasiyofaa kwa watoto.
Kanuni hizo zimetungwa ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Mawasiliano ya Kiektroniki na Posta ya Mwaka 2010.
Pia
imesema itaendelea kuhamasisha utengenezaji na uzalishaji wa maudhui ya
ndani yanayozingatia maadili, mila na desturi za Mtanzania huku ikikiri
kuwapo kwa mmomonyoko wa maadili kunakoongezeka siku hadi siku, hivyo
imejipanga kukabiliana na changamoto hiyo.
Akiwasilisha
bungeni mjini hapa jana hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Harrison
Mwakyembe, alisema kanuni hizo zinamtaka kila mtumiaji wa mitandao awe
na namba ya siri ili 'wajanja' wasitumie kirahisi chombo chake cha
mawasiliano kutenda matendo yanayokwenda kinyume cha sheria.
Alisema
kanuni hizo pia zinaweka muda maalumu kwa picha mgando na nyongevu za
filamu au muziki wenye maneno yasiyofaa kwa watoto kuonyeshwa kwenye
runinga.
"Tuliweka
muda huo maalumu kuanzia saa 4:00 usiku hadi saa 11:30 asubuhi, lakini
wadau wamekuwa wakali, wanadai picha na nyimbo hizo zirushwe kuanzia saa
6:00 usiku wakati watoto wamelala na mwisho saa 11:00 asubuhi, kabla
watoto hawajaamka," alisema Dk. Mwakyembe.
Aliongeza
kuwa kanuni hizo zinataka madaraja yawekwe kwa kila filamu, video,
wimbo au albamu kutoka ndani au nje ya nchi ndipo kazi hizo zitumike
kwenye vyombo vya utangazaji.
"Msingi
wa kanuni hizi ni kuhakikisha teknolojia inatutumikia badala ya
kututumikisha na kuvuruga mustakabali wa maadili ya taifa letu. Ni
kanuni zilizozingatia mazingira yetu halisi kama kila Watanzania,"
alisema.
Dk.
Mwakyembe alisema, mmomonyoko wa maadili ya Kitanzania unaoongezeka
siku hadi siku, ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili wizara yake.
Alisema
wanaendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na kuhamasisha jamii
kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili, mila na desturi za Kitanzania.
Ili
kutekeleza majukumu yake kwa mwaka ujao wa fedha, Dk. Mwakyembe
aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh. bilioni 33.3. Kati yake, Sh.
bilioni 12.2 ni mishahara, Sh. bilioni 9.3 kwa ajili ya matumizi mengine
na Sh. bilioni 8.7 za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Post A Comment: