Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro amefunguka na kudai anashukuru kuona baadhi ya wahalifu nchini wameanza kuelewa juu ya kauli yake ya 'uhalifu haulipi' huku akiendelea kuwasisitizia wengine ambao bado wanaendelea kujishughulishia na mambo hayo kuwa wasije kuilaumu serikali
IGP Sirro ametoa kauli wakati alipokuwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye kambi ya Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa lengo la kutaka kujua changamoto na hali walizokuwa nazo askari ndani ya kambi hiyo ili mradi aweze kushughulikia mapungufu atakayokumbana nayo.
"Mambo yanaweza yasiende vizuri sana kwa sababu kuna watu wengine wanataka waone wapi kuna upungufu ambapo askari hawafanyi kazi vizuri ili waweze kufanya uhalifu wao, na huwa ninasema siku zote uhalifu haulipi. Utapiga bunduki, utaiba leo, kesho ukiingia mahali pabaya usilaumu serikali", amesema IGP Sirro.
Aidha, IGP Sirro amesema sasa hivi kila mhalifu akitaka kuchukua bunduki kuenda kufanya tukio huwa anajiuliza mara mbili mbili kama ataweza kurudi salama huko aendapo, "Nashukuru sasa hivi wameanza kunielewa kwamba uhalifu haulipi", amesisitiza IGP Sirro.
Kwa upande mwingine, IGP Sirro amesema hapendi kumuona askari polisi akiwa legelege kwa kuwa akiwa hivyo atoweza kumlinda raia ipasavyo.
Post A Comment: