Baada ya kujihakikishia kupata zaid ya shilingi milioni 623 kutoka Shirikisho la Soka la Afrika (Caf), Yanga imeweka wazi mikakati ya matumizi ya fedha hizo watakavyozitumia.
Yanga imefanikiwa kuvuna fedha hizo baada ya kufanikiwa kuwaondoa wapinzani wao, Wolaitta Dicha ya Ethiopia kwa ushindi wa mabao 2-1 katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo kufuzu Hatua ya Makundi ya michuano hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika, ameliambia gazeti hili kuwa wamepanga kufanya kikao kizito cha viongozi wote na benchi la ufundi la timu hiyo litakaloongozwa na Mzambia, Noel Mwandila baada ya kurejea Dar.
Nyika alisema, lengo la kikao hicho ni kupanga bajeti ya matumizi ya fedha hizo ambazo kwa kuanzia watalipa madeni yote kutoka kwa wachezaji wao, ikiwemo mishahara na madai ya fedha za usajili wanazodaiwa.
Aliongeza kuwa, fedha hizo za Caf zitaongeza hamasa kubwa kwenye klabu yao kutokana na ukata ulioikumba timu hiyo katika kipindi hiki kigumu wakati ligi inaendelea.
“Ukweli upo wazi hata kama watani wetu Simba wanatukebehi, Yanga tulikuwa katika kipindi kigumu ambacho wachezaji wetu walikuwa wanacheza bila ya kulipwa mishahara hadi kufikia miezi mitatu.
“Pia, wapo baadhi ya wachezaji walikuwa wakicheza huku wakidai malipo ya fedha za usajili tangu msimu uliopita na mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo ni lazima tuwalipe ili tuanze mazungumzo mapya kwa ajili ya kusaini mikataba mipya.
“Na kingine kama unavyojua timu inapovuka kwenda hatua ya makundi inapewa nafasi (zisizozidi saba) za kusajili wachezaji, hivyo kwetu hilo lipo wazi kabisa ni lazima tusajili wachezaji katika kukiimarisha kikosi chetu ili kiwe imara na fedha zitakazotumika kusajili zitatumika hizi za Caf,” alisema Nyika.
Miezi kadhaa iliyopita, Caf ilifanya mabadiliko katika malipo kwa timu kwenye michuano inayosimamiwa na shirikisho hilo ambapo kulikuwa na ongezeko katika kila michuano, ambapo yataanza kutumia rasmi msimu huu ambao Yanga inashiriki.
Kiwango hicho cha 623m, Yanga wana uhakika watakipata hata kama watashika nafasi ya mwisho katika kundi, lakini watakavyofanya vizuri ndivyo ambavyo watakavyokuwa na nafasi kubwa ya kuingiza fedha nyingi zaidi hadi Sh bilioni 2.8 ikiwa watakuwa mabingwa.
Post A Comment: