KWA kila mtu anayemfahamu Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, msanii wa kizazi kipya ambaye kwa kipindi kirefu amekuwa akiipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa katika muziki, hawezi kuacha kushangazwa na kitendo cha msanii huyo kuposti video chafu, alichokifanya siku chache zilizopita.
Kwa ambao hawakupata nafasi ya kuzitazama video hizo, kwa nyakati tofauti Diamond alionekana akifanya hadharani mambo ya kikubwa, yanayopaswa kufanywa chumbani, tena kwa kificho, taa zikiwa zimezimwa, kibaya ni kwamba alikuwa pia akijirekodi.Ya kwanza alionekana akiwa na mwanamke mwenye asili ya kigeni, ambayo walikuwa wakiyafanya hayawezi kuandikika kwa lugha nyepesi, kwa kifupi ulikuwa ni uchafu ambao ni kinyume kabisa na mila za Kitanzania.
Hakuishia hapo, muda mfupi baadaye ikaonekana video nyingine akiwa na mzazi mwenzake, Hamisa Mobeto, wakifanya mambo yasiyofaa kuonekana hadharani, huku staa huyo wa ngoma ya African Beauty aliyomshirikisha msanii wa kimataifa, Omarion akionekana kugida pombe kwa fujo. Ukichunguza vizuri, inaonesha video zote mbili zilipigwa katika chumba kimoja, tena katika muda ambao haukupishana sana.
Unajaribu kujiuliza, lengo la Diamond kurekodi video hizo kisha baadaye kuziposti mitandaoni lilikuwa ni nini? Kutafuta kiki? Ina maana mpaka leo Diamond kwa levo alizofikia anaweza kuwa anategemea kiki kuendelea kubaki kwenye chati na kusahau kuna mamilioni ya vijana wanaomtazama kama ‘kioo’ chao? Alifanya kwa lengo la kumuumiza mzazi mwenzake, Zarina Hassan ‘Zari’ kwa lengo la kulipiza maumivu ya kuachwa? Unawezaje kumlipiza mwanamke aliyekuzalia watoto kwa utoto wa kiasi hiki?
Anataka kesho wanaye wakikua waje wajifunze nini kutoka kwa baba yao? Amesahau kwamba intaneti inao uwezo wa kuhifadhi mambo kwa miaka chungu mbovu kiasi kwamba hata wanaye watakuja kuona uchafu wa baba yao? Come on!
Namfahamu Diamond tangu akiwa anahangaika kutafuta njia ya kutokea katika gemu la Muziki wa Bongo Fleva na nilikuwa miongoni mwa waandishi wa mwanzomwanzo kuandika habari zake, Hemed Kisanda ambaye naye kwa kipindi hicho alikuwa mwandishi wa habari za burudani, anaweza kuwa shahidi mzuri wa hili.
Diamond wa kipindi hicho, siyo Diamond wa sasa, nakubali kwamba mafanikio hulevya lakini ulevi huu anaouonesha Diamond sasa ni ‘too much’, ni zaidi ya ulevi wa pombe haramu ya gongo. Mara kadhaa nakumbuka Diamond alikuwa akikatisha ‘intavyuu’ kwa lengo la kwenda kuswali baada ya kusikia adhana kwa sababu huyu ni muumini wa dini ya Kiislam, ziko wapi nyakati zile? Uko wapi unyenyekevu ule?
Sikia ‘A boy from Tandale’, hakuna hali ambayo huwa ni ya kudumu katika maisha, kama ule msoto wa enzi hizo ukiwa Tandale, ukisaga lami kutafuta promo ya kazi zako za muziki haukuweza kuwa wa kudumu maishani mwako baadaye ukatoboa, hata huu umaarufu ulionao sasa, wa kuruka na ndege kila kukicha, leo upo Ujerumani, kesho Marekani ukifanya shoo kubwa na kula bata, siyo kitu cha kudumu.
Mambo yote yatakapopita, matendo yako, utu wako na yale uliyowafanyia wengine ndiyo vitu vitakavyosalia, Waingereza wanasema ‘karma will hunt you’. Haya unayoyafanya leo, ipo siku yatakurudia, machozi ya wanawake unaowadhalilisha na kuwatumia kingono utakavyo, ipo siku yatakurudia na sijui kama utakuwa umejiandaa kukabiliana nayo, yanaweza yasikurudie wewe lakini yakaurudia uzao wako.
Matendo yako lazima yaendane na heshima unayopewa na mashabiki wako na watu wote wanaokutakia mema, wakiwemo viongozi wa nchi yetu! Umesahau ni siku chache tu zilizopita Rais Magufuli alikupa heshima kubwa kwenye uzinduzi wa Bombadier? Ukijikweza sana mbele za watu, ipo siku utashushwa mbele za watu na kila mmoja atakudharau! Na huu mchezo uliouanza hivi karibuni wa kutunishiana misuli na serikali, hauwezi kukuacha salama.
Adios Amigo.
Post A Comment: